
Na Mwandishi Wetu
Basi la abiria la Kampuni ya Nyehunge linalofanya safari kati ya Ngara, Biharamulo na Mwanza limepata ajali katika eneo la Nakatunga, kando ya Barabara Kuu ya Ngara–Kabanga.
Waandishi wa www.ngaratv.com walifika eneo la tukio na kushuhudia basi hilo likiwa limeanguka pembeni mwa barabara baada ya kupata ajali hiyo alfajiri ya leo.
Kwa mujibu wa mashuhuda, ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11:00 asubuhi wakati basi hilo likitoka Rulenge kuelekea Ngara Mjini kwa ajili ya kuchukua abiria kabla ya kuanza safari yake ya Mwanza.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa hakuna vifo vilivyoripotiwa kufuatia ajali hiyo. Hata hivyo, baadhi ya watu waliojeruhiwa walikimbizwa katika vituo vya afya kwa kutumia magari mengine yaliyokuwa karibu na eneo la tukio ili kupata matibabu.
Chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika rasmi, huku mamlaka husika zikitarajiwa kutoa taarifa zaidi baada ya uchunguzi kukamilika.
Ngara TV inaendelea kufuatilia kwa karibu tukio hilo na itawaletea wasomaji taarifa kamili pindi zitakapopatikana.
