TAHARUKI YA MOTO MKUBWA NGARA MJINI

By Na Mwandishi Jun 8, 2026


Hali ya taharuki ilitokea majira ya saa 8 mchana leo katika eneo la Nakatunga Kijiweni, Mjini Ngara, baada ya moto mkubwa kuzuka na kuunguza baadhi ya vibanda vilivyokuwa jirani na eneo hilo.


Kwa mujibu wa taarifa za awali, chanzo cha moto huo kinadaiwa kuwa ni uchomaji wa matairi karibu na gereji iliyopo eneo hilo. Moto huo ulisambaa kwa kasi na kusababisha hofu kwa wananchi waliokuwa karibu.


Jeshi la Uokoaji na Zimamoto Wilaya ya Ngara lilifika haraka eneo la tukio na kufanikiwa kuudhibiti moto huo kabla haujasababisha madhara makubwa zaidi.


Baadhi ya wananchi wamepongeza juhudi za askari wa zimamoto kwa mwitikio wao wa haraka uliofanikisha kudhibiti moto huo.

Aidha, wameishukuru Serikali kwa kuwezeshaupatikanaji wa gari la zimamoto wilayani humo, huku wakieleza kuwa bado kuna haja ya kuongeza magari mengine kutokana na ukubwa wa wilaya na uwepo wa maeneo mengi ya mipakani ikiwemo Kabanga, Rusumo, Murusagamba na Mugoma.


Hakuna taarifa rasmi zilizotolewa kuhusu idadi ya vibanda vilivyoteketea wala majeruhi kufuatia tukio hilo. Uchunguzi wa kina kuhusu chanzo halisi cha moto unaendelea.