
Na Juventus Juvenary Illambona & Nuru Christopher Nzoya – Ngara
Katika siku 30 za kwanza tangu aapishwe kuwa Mbunge wa Jimbo la Ngara, Mheshimiwa Dotto Jasson Bahemu ameendelea kuonyesha dira, nidhamu na utayari wa kuwahudumia wananchi kwa moyo wa dhati. Kauli nyingi kutoka kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ndani ya Jimbo la Ngara zinabainisha wazi kuwa kijana huyu ameanza vyema na anaonesha matumaini ya kuwa mwakilishi mahiri wa Wananchi wa Jimbo hilo.
Bahemu alichaguliwa kupitia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akiendeleza historia ya jimbo hilo ya kuwa na wabunge vijana, akifuatia mtangulizi wake Ndg Ndaisaba George Ruhoro (2020–2025).
Tarehe 11 Desemba 2025, Mbunge Bahemu ametimiza siku 30 tangu alipoapishwa rasmi kuwatumikia wananchi ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kipindi kifupi ambacho tayari kimeacha alama.
Katika siku hizi chache, Mheshimiwa Bahemu ameonyesha kwa vitendo namna anavyoweka mbele maslahi ya wananchi wa Ngara kupitia matukio na kazi mbalimbali, ikiwemo:
- Kukagua maendeleo ya Hospitali ya Wilaya ya Ngara (Mbuba) Ziara hii iliangazia uhitaji wa maboresho ya huduma za afya, miundombinu, madawa na vifaa tiba ikiwa ni ishara ya msukumo wake katika kuboresha ustawi wa wananchi.
2. Kuhamasisha michezo na kutimiza ahadi kwa wanamichezo Kupitia kutimiza ahadi na kutoa zawadi kwa wanamichezo katika ligi ya Mpira wa miguu Wilayani Ngara, ameonesha kuthamini vipaji na kujenga mazingira ya kuibua vijana wenye uwezo wa kuiletea heshima Ngara.
3. Kuandaa hafla ya kuwapongeza Madiwani na Wakuu wa Idara Kuwepo kwa Hafla hii kumejenga mshikamano kati ya uongozi wa Halmashauri na Jimbo, jambo ambalo ni muhimu katika kuharakisha maendeleo.
4. Kukabidhi gari la wagonjwa (Ambulance) kwa Hospitali ya Murgwanza Hii ni hatua iliyopokelewa kwa shangwe na wananchi, kama sehemu ya kuboresha huduma za dharura na usafiri wa wagonjwa akiwa anawakilisha serikali kwa ufanisi.
5. Kukutana na Uongozi wa Tembo Nickel
Katika hali ya uwakilishi na kutimiza jukumu alilopewa na wananchi wa Jimbo la Ngara, Mhe. Bahemu amefanya mazungumzo na Uongozi wa Tembo Nickel, ikiwa ni sehemu ya kusisitiza umuhimu wa fursa za kiuchumi zitokanazo na mradi huo kuwanufaisha moja kwa moja wananchi wa Jimbo la Ngara. Ni hatua ya muhimu sana katika kuwaunganisha wananchi wazawa na fursa zitakazotokana na uwepo wa Mgodi huu wenye mipango na uwekezaji wa muda marefu.
Mbali na majukumu ya kimkakati, Mheshimiwa Bahemu amehudhuria matukio ya kijamii ikiwemo sherehe, misiba na mikusanyiko mbalimbali. Aidha, amekuwa akikutana na vijana, wazee, viongozi wa dini na makundi tofauti tofauti akitengeneza uongozi unaosikiliza na kushirikisha jamii.
Siku 30 hizi zimekuwa kioo kinachoonyesha aina ya uongozi anaoujenga, uongozi wa karibu, wa vitendo na wenye mwelekeo makini kuelekea maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiutawala. Wananchi wengi wanaona hatua zake kama mwanzo wa safari ndefu yenye matumaini.
Kwa busara na unyenyekevu alionao Mhe. Bahemu, tunatambua na kupongeza juhudi zake. Ni wazi kuwa Ngara imepata kiongozi kijana mwenye nguvu, maarifa na dhamira ya dhati ya kulitumikia Jimbo.
