Police Services!

By admin Dec 26, 2025

Na Sam Ruhuza

Kwa muda mrefu nimekuwa nikiliomba hili kutokea,  leo namsikia Waziri wa Ndani akiliongelea! 

Juzi Mzee Warioba aliongelea hili la Police kuwa ndio wenye kutoa matamko ya utawala, Nchi kuongozwa Kipolice, Police State!! 

Kwanza tuelewe ni kwanini hali hii!? 

Kipindi cha Mkoloni, alianzisha Police kumlinda yeye Mtawala dhidi ya Raia, hivyo Police ilikuwa ikifanya kazi kwa maelekezo ya Mtawala! 

Baada ya Uhuru, Mtawala akawa mweusi mwenzetu na kutumia mfumo uleule wa Mkoloni kuendesha Police, japo kwa maneno linaonekana ni la wananchi, lakini kiutendaji, halipo huru! 

Police haruhusiwi kuwa mwanasiasa, lakini mfumo unamfanya mwanasiasa! 

Mkiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya,  Mkoa hadi Taifa ni wanasiasa, yaani DC, RC, Rais, hao wanakaa kwenye vikao vya chama, wanapewa maagizo na chama,kisha wanaita kikao chao na kutoa maelekezo kama Mkiti wa Kikao cha Ulinzi na Usalama. Hapo OCD, RPC na IGP  wanakuwa kwenye wakati mgumu kutofautisha maagizo ni ya Mkiti au ya Chama, anatakiwa kupiga salute na kwenda kutekeleza! Hakuna lolote Police anaweza kufanya kwa Raia bila maelekezo, ndio maana kumekuwa na kauli za maelekezo toka juu!! 

Police ni muhimu sana kwa Nchi, fikiria Nchi bila Police hata kwa nusu saa tu, tutakuwa kwenye hali gani mtaani?! 

Uwepo wa Police unatakiwa kutafsiri maana yake kwa jamii na sio vinginevyo! 

Bunduki anayoishika Police na Risasi zake, zimenunuliwa kwa kodi ya wananchi kumlinda yeye na Mali zake huku Mwananchi akimpa ushirikiano,  hatakiwi kuzitumia kumuumiza au kumuua Raia mwema kwasababu tu yeye ameshika silaha ambazo ni kodi yake! 

Police anatakiwa sana kuwa karibu na Raia na Raia amuamini popote anapokuwapo na Raia anapokuwa na Police asionekane ni mhalifu au ametekwa, anataka aonekane kama yupo na mtu sahihi kwa usalama! 

Ili tufikie huko ni lazima kubadilisha mfumo na wananchi waamini hayo mabadiliko ya mfumo na sio kubadilisha jina tu, maana hata Tume ya Uchaguzi ilibadilishwa jina na kuitwa Tume Huru ya Uchaguzi,  lakini Je, ni kweli  Tume Huru??! 

Mabadiliko ya mfumo yaambatane na 

– Ukomeshaji wa Utekaji! Watu wasiojulikana wakiendelea kusikika, haina maana tena, ni sawa na kusema bado kuna shida Police! 

– Watu waliopotea kwa kuchukuliwa na ‘watu wasiojulikana’ wapatikane au taarifa zao zijulikane, yaani wananchi kama vile Polepole na wengine! 

Hii itaanza kurudisha imani! 

– Police wanaohusishwa na matukio yaliyo kinyume na maadili,  watolewe na kuchukuliwa hatua! 

Hapo Mfumo utakwenda vyema.  

Mfumo mpya uwatenge kabisa wanasiasa kuingilia Police kwa namna yeyote ile, waachiwe wafanye kazi yao husika kwa ubora wao na nina imani wanaweza na watapenda iwe hivyo! 

Wananchi tunahitaji sana kufanya kazi na Police kwa maslahi ya Taifa, ila kwa hali ilivyo, ni lazima kwanza usafi ufanyike kurudisha imani ya Raia! 

Nimefurahi kusikia mabadiliko ya mfumo, lakini  ninasisitiza, lisiwe mabadiliko ya jina tu, bali liendane na usafishaji! 

Tanzania ni yetu sote! ðŸ‡¹ðŸ‡¿

By admin