KUOMBEA AMANI TAIFA

By Na Mwandishi Oct 22, 2025

‎DC NGARA:VIONGOZI WA DINI HUBIRINI AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU


‎Na,Juventus Juvenary-Ngara


‎Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Kanali Mathias Julius Kahabi, amewataka viongozi wa dini wilayani humo kusimama kidete kuhubiri amani wakati huu Taifa linapojiandaa kuelekea Uchaguzi Mkuu.


‎Akizungumza katika kikao maalum kilichowakutanisha viongozi wa dini, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau wa amani, Mkuu wa Wilaya ya Ngara Kanali Matias Julius Kahabi amesisitiza umuhimu wa kila mwananchi kushiriki kikamilifu kulinda amani ya nchi.


‎”Kila mmoja awe balozi wa mwenzake katika kuitunza na kuilinda amani ya nchi,” alisema DC Kahabi.


‎Aidha, alisisitiza umuhimu wa wananchi waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi kupiga kura, huku akiwatahadharisha vijana dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.


‎”Ninawakemea vikali baadhi ya vijana wanaotumia mitandao ya kijamii kusambaza matusi na ujumbe usio na maadili dhidi ya viongozi. Hili halikubaliki,” aliongeza.


‎Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ngara, Kamanda William Solla, alisisitiza kuwa uhalifu wowote unaolenga kuvuruga amani hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa uzito wake.


‎“Kosa la jinai halina ukomo. Watakaoshiriki vitendo vya uvunjifu wa amani watachukuliwa hatua kali za kisheria,” alionya Kamanda Solla.


‎Aliwataka viongozi wa dini kuhakikisha ujumbe waliopokea katika kikao hicho unawafikia waumini wao ili kwa pamoja kulinda misingi ya amani.


‎Nye Mgombea Ubunge Jimbo la Ngara,Dotto Jasson Bahmu ambaye alishiriki kikao hicho, alitoa ushuhuda wake na wito kwa jamii akisema “Nina miaka 37 na mtoto wangu wa kwanza ana miaka 11. Tunaishi kwa amani iliyorithiwa kutoka kwa wazee wetu. Ni jukumu letu sote kuilinda.”


‎Dotto alisisitiza kuwa uchaguzi ni haki ya kikatiba na si chanzo cha migogoro, hivyo Watanzania wote wanatakiwa kuungana pamoja kulinda amani,kuwa na upendo mshikamano na kuheshimu mamlaka zilizopo.


‎”Tuwakatae wote wenye nia ya kuchonganisha na kuvuruga amani ya nchi kwa kuhamasisha maandamano yenye madhara.” alisema Dotto Jasson Bahemu.


‎Viongozi wote wa Dini waliohudhuria kikao hicho, wamekubaliana kwa pamoja kuilinda Amani ya Nchi na kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga Kura Oktoba 29,mwaka huu kuwachagua madiwani, Mbunge na Rais.