Na, Juventus Juvenary -Rulennge.
Mbunge wa Jimbo la Ngara, Dotto Jasson Bahemu, amewataka wananchi kujenga na kudumisha tabia ya kushukuru mara baada ya kufanikisha jambo lolote muhimu katika maisha yao.
Bahemu ametoa kauli hiyo wakati wa salamu zake kwa wananchi, viongozi wa dini na viongozi wa kisiasa waliohudhuria dua maalum iliyoandaliwa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Bi. Samira Khalfan.
Tukio hilo limefanyika Desemba 18 nyumbani kwa Bi. Samira Khalfan, katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Rulenge.
Katika salamu zake, Mbunge Bahemu amempongeza Bi. Samira kwa kuandaa tukio hilo muhimu lenye lengo la kuwashukuru wananchi walioshiriki katika Uchaguzi Mkuu uliopita na kumchagua kuwa Mbunge wa Viti Maalum, pamoja na kuandaa dua maalum ya kuwaombea wazee.
“Ni wachache sana wanaokumbuka kushukuru baada ya kufanikisha mambo yao. Hivyo, tukio hili liwe funzo kwetu sote la kujenga utamaduni wa kushukuru,” alisema Bahemu.
Aidha, Mbunge huyo ambaye yupo jimboni kuendelea na ziara pamoja na utekelezaji wa majukumu mbalimbali, amesema anatarajia kufanya mkutano mkubwa wa kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Ngara ndani ya kipindi cha wiki mbili zijazo.


