UBINAFSI WATAJWA KUCHOCHEA UKATILI KWA WATOTO NGARA

By Na Mwandishi Apr 13, 2026

Wadau wataka ushirikiano wa jamii kukomesha vitendo vinavyohatarisha malezi bora

Na Mwandishi Wetu, Ngara

Jamii imetakiwa kuachana na tabia ya ubinafsi na badala yake kushirikiana kwa pamoja katika kupinga ukatili dhidi ya watoto, hali inayotajwa kuhatarisha ustawi na maendeleo yao.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la EDFO, Bw. Noel Kihoza, wakati akifungua kikao cha wadau kilicholenga kudhibiti ukatili kwa watoto katika kata za Keza, Rulenge na Nyakisasa, wilayani Ngara mkoani Kagera.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Nzeyi, uliopo Mamlaka ya Mji Mdogo wa Rulenge, Bw. Kihoza alisema kuwa mapambano dhidi ya ukatili hayawezi kufanikiwa iwapo jamii itaendelea kuwa na mtazamo wa kujali maslahi binafsi badala ya ustawi wa pamoja.

“Ni wakati wa jamii kubadilika na kushirikiana kwa dhati kulinda haki za watoto wetu, kwani wao ndio msingi wa taifa la kesho,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wilayani Ngara, Bw. Peter John, alieleza kuwa hali ya ukatili bado ni changamoto kubwa, akibainisha kuwa watoto 114 wameathiriwa na vitendo vya ukatili katika kipindi cha miezi mitatu pekee kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.

Aliongeza kuwa takwimu hizo zinaonesha haja ya hatua za haraka na shirikishi ili kupunguza na hatimaye kutokomeza vitendo hivyo.

Naye Afisa Mradi wa Kupinga Ukatili kutoka Shirika la CODISO, Bw. Nuru Christopher Nzoya, alisema kuwa kuanza kwa mradi mpya wa kupinga ukatili kunaleta matumaini ya kubadilisha mtazamo wa jamii.

Alieleza kuwa kupitia elimu na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali, jamii inaweza kufikia hatua ya kukomesha kabisa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

Hatua hiyo imekuja wakati ambapo wadau wa maendeleo wanazidi kusisitiza umuhimu wa kulinda haki za mtoto ili kuhakikisha wanakua katika mazingira salama na yenye kuwajengea uwezo wa kufikia ndoto zao