Ngara, Kagera
Wananchi wa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera wameiomba Serikali kuona umuhimu wa kuanzisha safari rasmi za ndege za abiria angalau mara mbili kwa wiki kutoka Ngara kwenda Mwanza au ikiwezekana safari ya moja kwa moja hadi Dar es Salaam, wakiamini hatua hiyo itachochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazetili hi, Bi. Zawadi Paschal mkazi wa Kijiji cha Mukididiri, Joseph Misago wa Kabanga pamoja na January Marton wa Kanazi wamesema uwepo wa huduma ya usafiri wa anga utarahisisha safari za wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kwa ujumla.
Wamesema Wilaya ya Ngara ina fursa ya kipekee kutokana na kuwa karibu na mipaka ya nchi za Rwanda na Burundi, huku pia ikihudumia wageni kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.
Kwa mtazamo wao, Ngara inaweza kuwa kitovu cha usafiri wa anga kwa ukanda huo iwapo safari za abiria zitaanzishwa.
Kwa sasa, Kiwanja cha Ndege cha Ruganzo hutumika zaidi kwa safari maalum, zikiwemo zinazohusiana na shughuli za kampuni ya uchimbaji madini ya Tembo Nickel Corporation pamoja na safari za viongozi wa Serikali.
Wananchi hao wanaamini kuwa kuanzishwa kwa safari za kibiashara kutainua sekta za biashara, utalii na uwekezaji, pamoja na kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri kupitia shughuli za uwanja wa ndege na huduma zake.
Aidha, wametoa wito kwa viongozi wa Wilaya na Mkoa, akiwemo Mbunge wa Jimbo la Ngara Dotto Jasson Bahemu, kulichukulia suala hilo kama kipaumbele cha maendeleo na kulifikisha katika ngazi husika za maamuzi Serikalini.
Wamesema kuwa iwapo tathmini ya kitaalamu itafanyika na kuonesha uwezekano wa huduma hiyo, basi Ngara inaweza kufungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wake na ukanda mzima wa Maziwa Makuu.

