VITAMBULISHO VYA NIDA NGARA YAZUA MALALAMIKO MAKUBWA

By Na Mwandishi Apr 26, 2026


Wananchi wamuomba Mbunge kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani.


Ngara, Kagera — Wananchi wa Wilaya ya Ngara wameelezea kuchoshwa na changamoto zinazowakabili katika zoezi la uandikishaji wa Vitambulisho vya Taifa vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), wakidai utaratibu unaotumika umekuwa kikwazo kikubwa kwao kupata huduma hiyo muhimu.
Baadhi ya wananchi wamehoji hali hiyo kwa masikitiko wakisema inawafanya wajisikie kama wageni ndani ya nchi yao. “Inafika hatua unajiuliza, Ngara bado ni sehemu ya Tanzania au ni kama kambi ya watu fulani tu?” alihoji mwananchi mmoja aliyekataa kutajwa jina.
Wananchi hao wanasema wanalazimika kupanga foleni kwa muda mrefu, hali inayosababisha kupoteza muda wa kufanya shughuli za uzalishaji na maendeleo ya familia zao. Wameeleza kuwa wakati mwingine hulazimika kusubiri siku nzima bila kuhudumiwa.
Aidha, malalamiko makubwa yameelekezwa kwa maafisa wa Idara ya Uhamiaji Tanzania wanaoshiriki katika uhakiki wa taarifa, ambapo baadhi ya wananchi hudai kuwekewa alama ya “C” kwenye fomu zao — ishara ya kuwa na mashaka ya uraia, jambo linalosababisha kucheleweshwa kwa huduma hadi uchunguzi zaidi ufanyike.
Wananchi hao wanahoji mantiki ya hatua hiyo, wakisema baadhi yao ni wazawa wanaofahamika katika jamii, wakiwemo viongozi na wasomi. “Inashangaza kuona mtu mzawa kabisa anawekewa alama ya mashaka, wakati historia yake inajulikana wazi,” alieleza mkazi mwingine.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wamemuomba Mbunge wa Jimbo la Ngara kuingilia kati suala hilo kwa kuwasiliana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kupata ufafanuzi na suluhisho la kudumu kuhusu utaratibu huo.
Katika hatua nyingine, mkazi mmoja wa Kata ya Kasulo amesema kuwa jana watu wawili walizimia kutokana na uchovu uliotokana na kusubiri kwa muda mrefu kwenye foleni, na kulazimika kupelekwa hospitali kwa matibabu.
Wananchi wameitaka serikali kuboresha utaratibu wa uandikishaji, kuongeza watumishi na vifaa, pamoja na kuweka mfumo rafiki utakaowawezesha kupata vitambulisho hivyo bila usumbufu mkubwa.