Mbunge Dotto Bahemu Ahimiza Wananchi Kuendelea Kuliombea Amani Taifa

By Na Mwandishi Jul 29, 2026

Mbunge wa Jimbo la Ngara, Mhe. Dotto Jasson Bahemu, ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kuliombea amani Taifa, ili kuliepusha na migogoro mbalimbali ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Mhe. Dotto ametoa wito huo leo Jumatano, Julai 29, 2026, katika Ibada ya Kipaimara, iliyofanyika katika Kanisa la Anglikana Dinari ya Murugarama, iliyoongozwa na Askofu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Kagera, Mhashamu Darlington Bendankeha.

Amesema ni muhimu kuliombea amani Taifa la Tanzania, kwani amani iliyopo ndiyo inayoleta umoja na uhuru wa Watu kujitafutia kipato, na kwamba endapo amani hiyo itatoweka basi Wananchi watalazimika kuishi ugenini katika Mataifa mengine wakiwa Wakimbizi.

Kwa upande wake Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Kagera, Mhashamu Darlington Bendankeha, amempongeza Mbunge kwa namna ambayo amekuwa akizungumzia maendeleo ya Jimbo la Ngara ndani na nje ya Bunge, na kwamba wao wataendelea kuliombea amani Taifa pamoja na Viongozi wake akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Naye Askofu Mstaafu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Kagera, Dkt. Aron Kijanjali, amempongeza Mbunge kwa kuanza vyema katika kuliwakilisha Jimbo la Ngara, na kuwasihi Wananchi kumpa ushirikiano katika kufanikisha azma ya kuleta maendeleo katika Jimbo la Ngara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *