MRADI WA TEMBO NICKEL WAPATA MWANGA MPYA NGARA

By Na Mwandishi Apr 28, 2026


Na, Juventus Juvenary.
Wananchi wa Jimbo la Ngara Mkoani Kagera wamepata matumaini mapya kufuatia hatua nzuri iliyofikiwa katika mchakato wa kuanza kwa Mradi wa Uchimbaji wa Nickel unaotarajiwa kutekelezwa na kampuni ya Tembo Nickel Corporation.

Akizungumza Bungeni jijini Dodoma wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/27, Mbunge wa Jimbo la Ngara, Mheshimiwa Dotto Jasson Bahemu, alisisitiza umuhimu wa kuanza kwa mradi huo haraka ili kufungua fursa za ajira na kukuza uchumi wa wananchi.

Mhe. Bahemu alieleza kuwa wananchi wa Ngara wamekuwa na matarajio makubwa juu ya mradi huo, hivyo ni muhimu sasa kuona utekelezaji wake ukianza kwa vitendo.

Alibainisha kuwa mradi huo una uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha ya wananchi kupitia ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, pamoja na kuchochea maendeleo ya miundombinu katika eneo hilo.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alithibitisha kuwa maandalizi ya mradi yanaendelea vizuri na yako katika hatua ya kuridhisha.

Aidha, aliahidi kufika wilayani Ngara hivi karibuni kwa ajili ya kuzungumza na wananchi na kuwapa taarifa ya kina kuhusu hatua zilizofikiwa.

Ahadi hiyo imepokelewa kwa matumaini makubwa na wananchi, ambao sasa wanasubiri kwa hamu kuona utekelezaji wa mradi huo ukianza rasmi na kuleta mabadiliko chanya katika maisha yao.

Mradi wa Tembo Nickel unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati itakayochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya madini nchini, huku Wilaya ya Ngara ikitajwa kuwa kitovu kipya cha fursa za kiuchumi Kanda ya Ziwa.