MASHINDANO YA POLISI JAMII KUTIMUA VUMBI NGARA HADI JULAI 25

By Na Mwandishi Jul 10, 2026


Mashindano ya Polisi Jamii yanatarajiwa kuendelea kutimua vumbi katika Wilaya ya Ngara hadi Julai 25, 2026, yakihusisha timu mbalimbali kutoka maeneo tofauti kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi kupitia michezo.


Mashindano hayo yanapata nguvu kupitia ushirikiano wa wadau mbalimbali, akiwemo Mbunge wa Jimbo la Ngara, Mheshimiwa Dotto Jasson Bahemu, ambaye ametoa msaada wa mipira na vipenga kwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Ngara ili kuwezesha uendeshaji mzuri wa mashindano hayo.


Vifaa hivyo vilikabidhiwa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ngara kwa niaba ya Mheshimiwa Dotto Jasson Bahemu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake ya kuunga mkono mashindano ya Polisi Jamii na kuendeleza michezo kama nyenzo ya kuimarisha uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.


Mazungumzo hayo yalifanyika wakati wa makabidhiano hayo kati ya Katibu Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Ngara, Juventus Juvenary Illambona, na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ngara ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kabanga, Bw. Hafidh Abdalla, kwa upande mmoja, na Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Ngara, ACP Machumu Jeremia, kwa upande mwingine.


Katika mazungumzo hayo, ACP Machumu Jeremia alisema mashindano yatafanyika kwa mfumo wa tarafa ili kutoa fursa kwa wananchi wengi kushiriki na kuendeleza dhana ya Polisi Jamii. Alieleza kuwa Wilaya ya Ngara ina tarafa nne ambazo zitashiriki katika mashindano hayo, ambazo ni Nyamiaga, Kanazi, Rulenge na Murusagamba.

Kila tarafa itashindanisha timu zake, huku washindi wakisonga mbele hadi hatua za mwisho za mashindano.


Amesema lengo la mashindano hayo si kuibua vipaji vya michezo pekee, bali pia kuimarisha uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, kuhamasisha ulinzi shirikishi na kudumisha amani, usalama na utulivu katika Wilaya ya Ngara.


Wananchi wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia michezo hiyo na kuendelea kudumisha amani, nidhamu na ushindani wa haki hadi kilele cha mashindano hayo kitakachofanyika Julai 25, 2026.