
Elie Mpanzu ameibuka shujaa wa Simba SC baada ya kufunga bao la ushindi na kuipa timu yake ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya watani wao wa jadi, Young Africans (Yanga), katika Dabi ya Kariakoo iliyowasha moto wa ushindani ndani na nje ya uwanja.
Yanga walianza kwa kishindo, wakipata bao kupitia Peter Shalulile dakika ya tano, lakini Simba hawakukubali kutawaliwa na matokeo hayo.
Wekundu wa Msimbazi walirejea kipindi cha pili kwa kasi na dhamira ya kusaka ushindi, Neo Maema akisawazisha dakika ya 68 kabla ya Mpanzu kupigilia msumari dakika ya 72.
Bao la Mpanzu limekuwa pigo kwa Yanga na furaha kubwa kwa mashabiki wa Simba, huku winga huyo akionyesha thamani yake katika mchezo wenye presha kubwa. Kufunga bao linaloamua hatima ya dabi kunamweka kwenye mjadala wa kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi.
Kwa upande wa Simba, ushindi huo ni zaidi ya pointi tatu; ni fahari ya kuwazidi watani wao katika pambano ambalo kila nafasi ina uzito wake. Yanga, kwa upande mwingine, italazimika kujitathmini baada ya kushindwa kulinda uongozi na kuruhusu mchezo kugeuka ndani ya kipindi kifupi.M
Kwa wapenzi wa Michezo lugha rahisi inayoweza kuzungumzwa ni “PANZU AMESEMA YAKE UWANJANI!”.
Bao moja la ushindi, dabi imechukuliwa na Wekundu wa Msimbazi wameondoka na tabasamu.
Kwa matokeo hayo SIMBA 2-1 YANGA, SC imekaa kileleni kwenye Ligi ikiongoza kwa alama 21 huku Yanga wakifuata kwa alama 18.
