Na Mkebe wa Chuma | Mbinga, Ruvuma

Nilipokuwa mjini Mbinga, mkoani Ruvuma, nilikutana na mama mmoja wa makamo aliyeniuliza kama nilikuwa nimesikia taarifa za ajali ya Morogoro iliyodai maisha ya Watanzania zaidi ya 30.
Nilipomjibu ndiyo, alitamka maneno yaliyoniacha nikiwa kimya.
“Vifo ni vifo tu. Kinachoniumiza ni vifo vya raia, lakini hao maaskari, acha walipe madeni yao.”
Kwa uchungu zaidi, alifichua kuwa naye alipoteza mdogo wake Oktoba 29.
“Kaka yangu, nina uchungu sana. Mdogo wangu aliuawa na hao hao maaskari. Acha nao wafe!”
Nilibaki na maswali mengi moyoni. Ni maumivu ya kiwango gani yanayoweza kumfanya mtu afikie hatua ya kutohuzunishwa na kifo cha mwingine?
Baadaye, niliposoma maoni ya Watanzania kwenye mitandao ya kijamii kufuatia vifo vya baadhi ya askari katika ajali hiyo, nilitafakari zaidi.
Nyuma ya baadhi ya kauli hizo kuna majeraha, hasira na maumivu ambayo hayawezi kupuuzwa.
NCHI INALIA. WANANCHI WANAUGULIA MAUMIVU MIOYONI MWAO.
Hata hivyo, kifo hakipaswi kuwa kisasi, wala maumivu ya mtu mmoja hayapaswi kuwa furaha ya mwingine.
Kila uhai una thamani. Pale madai ya dhuluma yanapokuwepo, haki na uwajibikaji ndiyo njia ya kurejesha imani.
Huenda kilio cha Watanzania kisiwe cha aina moja, lakini kinapaswa kutuamsha na kutufanya tutafakari kuhusu haki, utu na amani ya taifa letu.
Mwenyezi Mungu awafariji wote waliopoteza wapendwa wao na aturejeshee faraja inayostahili jina letu zuri la Tanzania.
