POLISI JAMII BODABODA RULENGE WASHUKA DIMBANI LEO KWA MAANDALIZI YA MTANANGE DHIDI YA MURUSAGAMBA

By Na Mwandishi Jul 14, 2026

Timu ya Polisi Jamii Bodaboda Rulenge leo, Julai 14, 2026, inatarajiwa kushuka dimbani kupambana na White Horse katika mchezo wa kirafiki unaolenga kukiimarisha kikosi kuelekea mchezo muhimu dhidi ya Polisi Jamii Murusagamba, utakaopigwa Julai 19, 2026.

Mchezo wa leo ni sehemu ya maandalizi ya mwisho ya timu, huku benchi la ufundi likitarajia kuwapima wachezaji, kuimarisha mbinu za ushambuliaji na ulinzi pamoja na kuongeza uimara wa kikosi kabla ya kukutana na wapinzani wao wa Murusagamba.

Mashindano haya yanaandaliwa kama sehemu ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Polisi Jamii, yatakayofanyika tarehe 25 Agosti, 2026. Kupitia michezo, Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha falsafa ya Polisi Jamii kwa kujenga mahusiano bora na wananchi, kuhamasisha amani, mshikamano, uzalendo na ushiriki wa jamii katika kudumisha usalama.

Wananchi wa Rulenge na maeneo ya jirani wanahamasishwa kujitokeza kwa wingi uwanjani kuishangilia timu yao na kuendelea kuunga mkono juhudi za Polisi Jamii zinazotumia michezo kama daraja la kuimarisha umoja na ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.

Michezo huunganisha jamii, huku Polisi Jamii ikiendelea kujenga Tanzania yenye amani, usalama na mshikamano.