RAIS SAMIA ATANGAZA SAFARI MPYA YA AIR TANZANIA KUELEKEA URUSI

By Na Mwandishi Jun 5, 2026


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametangaza rasmi kuanza kwa safari mpya ya Shirika la Ndege la Tanzania, Air Tanzania, itakayokuwa ikisafiri kati ya Dar es Salaam, Zanzibar na Urusi.


Rais Samia ametoa tangazo hilo Juni 5, 2026 wakati akihutubia Kongamano la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg International Economic Forum nchini Urusi, kabla ya kuhitimisha ziara yake maalum katika taifa hilo.


Amesema kuanzishwa kwa safari hiyo mpya kutaimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi kwa kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa, sambamba na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii na biashara.


Rais Samia pia ameeleza matumaini yake kwamba shirika la ndege la Urusi, Azur Air, litaanza safari za moja kwa moja kutoka Urusi kwenda Zanzibar, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania na kufungua fursa zaidi za uwekezaji na biashara.


Hatua hizi ni sehemu ya jitihada za Tanzania na Urusi za kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kufikia malengo ya maendeleo ambayo mataifa hayo mawili yamejiwekea kupitia ushirikiano katika sekta mbalimbali.