WANANCHI BUGARAMA WAJITOKEZA KUNUFAIKA NA MPANGO WA REA WA UUZWAJI MITUNGI YA GESI

By Na Mwandishi May 28, 2026


Na, Ramadhan Kabaheza – The Ngara Finest

Wananchi wa Kata ya Bugarama, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, wamejitokeza kwa wingi kunufaika na mpango wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wa usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia kwa bei nafuu ya shilingi 17,500 pekee.


Wananchi hao walifika katika kituo cha muda kilichowekwa eneo la Bugarama Center kwa ajili ya usajili na ugawaji wa mitungi hiyo, hatua inayotajwa kuwa mwanga mpya kwa familia nyingi za vijijini katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.


Baadhi ya wananchi waliojitokeza wameeleza kufurahishwa na mpango huo wakisema utasaidia kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao umekuwa ukichangia uharibifu wa mazingira pamoja na changamoto mbalimbali za kiafya katika familia nyingi.


Wamesema matumizi ya kuni husababisha ukataji mkubwa wa miti na kuongeza hatari ya mabadiliko ya tabianchi, huku moshi unaotokana na kuni na mkaa ukiendelea kuwa chanzo cha magonjwa ya mfumo wa upumuaji, matatizo ya macho pamoja na athari nyingine za kiafya, hasa kwa wanawake na watoto wanaokaa muda mrefu jikoni.


Aidha, wananchi hao wamebainisha kuwa matumizi ya gesi ni rahisi, yanapunguza muda wa kupika, yanaweka mazingira safi ndani ya nyumba na kusaidia kuokoa muda uliokuwa ukitumika kutafuta kuni.


Hata hivyo, baadhi yao wameomba kuwepo kwa kituo cha kudumu cha kujazia gesi katika eneo la Bugarama au maeneo ya karibu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo pale gesi zinapoisha, wakisema umbali wa kufuata huduma unaweza kuwa changamoto kwa wananchi wengi wa vijijini.


Mpango wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi unaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata nishati bora, salama na rafiki kwa mazingira.