Wadai Elimu ya Usalama Barabarani.
Na Mwandishi Wetu-Ngara.
Wananchi wanaoishi kandokando ya barabara ya kutoka Nyamiaga hadi Feri wameiomba Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka kutoa elimu ya usalama barabarani kufuatia kuongezeka kwa vitendo vya uendeshaji hatarishi.Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema baadhi ya madereva wageni, hususan kutoka nchi jirani ya Burundi, wanakiuka sheria za barabarani ikiwemo kushindwa kufuata upande sahihi wa kupita, hali inayoweka maisha ya watumiaji wa barabara hiyo hatarini.Mmoja wa wananchi hao, Mussa Imani, amesema hali ya usalama barabarani imekuwa ya kutisha kutokana na uendeshaji usiozingatia sheria.“Tunaiomba Polisi waje watoe elimu kwa hawa wageni wetu, maana wanaendesha kwa fujo na hawazingatii kabisa sheria za barabarani,” amesema Imani.Kwa upande wake, Minanagi Samson amesema uwekaji wa alama za barabarani unaweza kusaidia kupunguza ajali, hasa katika maeneo yenye kona kali.“Barabara hii haina alama za kutosha, hasa kwenye kona. Kama zitawekwa, zitasaidia madereva kuwa makini zaidi,” amesema Samson.Naye dereva wa bodaboda, Kulwa Yohana, amesema madereva wanaoendesha bila tahadhari wamekuwa tishio kwa waendesha pikipiki na watembea kwa miguu.“Sisi waendesha bodaboda tupo hatarini sana. Kuna wakati magari yanakuja kwa kasi bila hata kufuata upande, ni rahisi sana kugongwa,” amesema Yohana.Hivi karibuni, watu wawili walinusurika kugongwa katika eneo la Murunyinya baada ya gari lililokuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi kupita bila tahadhari.Wananchi hao wameiomba Serikali na mamlaka husika kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa, ikiwemo utoaji wa elimu ya usalama barabarani na uwekaji wa alama muhimu ili kulinda maisha ya watumiaji wa barabara hiyo.



