Na Ramadhan Kabaheza, Ngara
Chama cha ushirika cha wakulima wa zao la kahawa wilayani Ngara mkoani Kagera, Ngara Farmers, kimeahidi kuhakikisha kinatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima wa zao hilo ili kuongeza uzalishaji na kipato chao.
Akizungumza katika mkutano na wakulima wa Kijiji cha Bugarama, mmoja wa viongozi wa chama hicho, Bw. Jeremia Philipo Tembo, amesema hakuna sababu tena kwa mkulima wa kahawa kuendelea kupata tabu kutokana na changamoto za pembejeo na ukosefu wa fedha za maandalizi ya mashamba.
Amesema chama hicho kimeanzisha utaratibu wa kutoa fedha za uwezeshaji kwa wakulima, ambapo mkulima ataweza kuomba mkopo kulingana na historia yake ya mauzo ya msimu uliopita.
Amefafanua kuwa mkulima atajidhamini kwa kutumia kitambulisho cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na kuthibitishwa na kiongozi wa kijiji au kitongoji ili kupata fedha za kukidhi mahitaji yake wakati akisubiri msimu wa mauzo na malipo.
Kwa upande wake, mwakilishi wa UBUMWE na kiongozi wa Ngara Farmers katika Kijiji cha Bugarama, Bw. Jafar Said, amewahimiza wakulima kujiunga na ushirika huo ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na chama hicho.
Aidha, amewatahadharisha wakulima wanaojiunga na vyama zaidi ya kimoja kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha utaratibu na kunaweza kusababisha matatizo ya kisheria pamoja na kukosa sifa za kupata huduma zinazotolewa.
Naye mkulima wa kijiji hicho, Bw. Charles Barimpaka, amelalamikia changamoto zinazoendelea kuwakabili wakulima, ikiwemo ukosefu wa pembejeo na mitaji ya kuendesha shughuli za kilimo, na kuiomba Serikali pamoja na wadau wa kilimo kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto hizo.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Kata ya Bugarama, Bw. Kamugisha, amewahimiza wakulima hususan vijana kuanza mapema maandalizi ya mashamba ili waweze kunufaika na ugawaji wa miche pamoja na msaada wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa kilimo.
Wakulima wa Bugarama wameeleza matumaini yao kuwa kupitia juhudi hizo, wataweza kuongeza uzalishaji wa kahawa na kuboresha kipato chao, hali itakayochangia maendeleo ya Wilaya ya Ngara kwa ujumla.





