UKIRITIMBA WA MGAO WA MAJIKO YA RUZUKU WADAIWA KUKWAMISHA WANANCHI NGARA

By Na Mwandishi Jun 2, 2026


Na Mwandishi Wetu, Ngara


Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera wamelalamikia kile wanachodai kuwa ni ukiritimba katika zoezi la ugawaji wa majiko ya ruzuku, hali ambayo imeelezwa kuwanyima fursa ya kunufaika na mpango huo wa Serikali unaolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.


Kwa mujibu wa wananchi hao, matangazo yanayotolewa yanaeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mpango wa kusambaza majiko ya ruzuku ili kuhamasisha matumizi bora ya nishati na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.


Wananchi hao wamesema kuwa Wilaya ya Ngara ipo katika awamu ya pili ya ugawaji wa majiko hayo, ambapo awamu ya kwanza ilihusisha majiko yanayotumia mkaa, huku awamu ya sasa ikihusisha majiko yanayotumia gesi.


Hata hivyo, wameeleza kuwa mawakala wanaosimamia usambazaji wa majiko hayo wamekuwa wakichukua majina na namba za vitambulisho vya Taifa (NIDA) za wananchi wengi, wakiwemo baadhi ya madiwani, lakini baadhi yao hawapati majiko hayo baada ya kukamilisha taratibu zilizotakiwa.


“Tunajisajili na kutoa taarifa zote zinazohitajika, lakini mwisho wa siku tunaambiwa majiko yameisha. Hali hii inatukatisha tamaa na kutufanya tuhisi kuwa kuna upendeleo katika ugawaji,” alisema mmoja wa wananchi aliyeshiriki zoezi hilo.
Wananchi hao wameongeza kuwa mara nyingi hulazimika kupanga foleni kwa muda mrefu wakisubiri huduma, lakini baadaye hupewa taarifa kuwa idadi ya majiko yaliyopo imekwisha, jambo linalozua maswali kuhusu uwazi wa mchakato huo.


Kutokana na hali hiyo, wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Nishati na mamlaka husika kuingilia kati ili kuhakikisha ugawaji wa majiko ya ruzuku unafanyika kwa uwazi, haki na usawa kwa wananchi wote waliolengwa na mpango huo.


Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, majiko ya mkaa yanayotolewa kwa ruzuku yanauzwa kwa shilingi 12,500 huku majiko ya gesi yakiuzwa kwa shilingi 17,500.


Wananchi wamesema kuwa mpango huo una manufaa makubwa katika kuboresha matumizi ya nishati safi, lakini wameitaka Serikali kufuatilia utekelezaji wake ili kuhakikisha lengo lililokusudiwa linafikiwa na walengwa wote.