WAUMINI WA BUHORORO WAUNGANA NA WAKATOLIKI WOTE DUNIANI KUADHIMISHA SIKUKUU YA EKARISTI TAKATIFU

By Na Mwandishi Jun 7, 2026


Na Juventus Juvenary Illambona


Waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Buhororo leo wameungana na Wakatoliki wote duniani kuadhimisha Sikukuu ya Ekaristi Takatifu, ambayo ni miongoni mwa sikukuu muhimu katika maisha na imani ya Kanisa Katoliki.


Maadhimisho hayo yamefanyika huku waamini wakikumbushwa umuhimu wa Ekaristi Takatifu kama kitovu cha maisha ya Kikristo na ishara ya uwepo halisi wa Yesu Kristo katika Kanisa.


Kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa Katoliki, kuabudu Sakramenti Tukufu kunatokana na imani kwamba Yesu Kristo yupo hai, kweli na kikamilifu katika Ekaristi Takatifu.

Msingi wa imani hiyo unatokana na maneno ya Yesu Kristo aliyoyatoa wakati wa Karamu ya Mwisho aliposema: “Huu ndio mwili wangu… Hii ndiyo damu yangu” (Mathayo 26:26–28).


Tangu nyakati za Mitume, Wakristo walikusanyika kuumega mkate na kuadhimisha Ekaristi wakiamini kuwa wanakutana na Kristo aliye hai. Kadiri miaka ilivyopita, Kanisa liliendelea kutafakari kwa kina fumbo hilo na kuimarisha heshima kwa Sakramenti Tukufu.


Historia inaonesha kuwa mwaka 1264, Papa Urban IV alianzisha rasmi Sikukuu ya Mwili na Damu ya Kristo (Corpus Christi) kwa Kanisa lote, hatua iliyosaidia kueneza ibada ya kuabudu Sakramenti Tukufu katika maeneo mbalimbali duniani.


Kanisa linafundisha kuwa kuabudu Sakramenti Tukufu si kuabudu mkate, bali ni kumwabudu Yesu Kristo mwenyewe ambaye Wakatoliki wanaamini yupo chini ya maumbo ya mkate na divai.

Kutokana na imani hiyo, waamini husali, hutafakari na kuonesha heshima kubwa mbele ya Sakramenti Tukufu.


Maadhimisho ya mwaka huu yamekuwa fursa kwa waamini wa Parokia ya Buhororo kutafakari upya nafasi ya Ekaristi katika maisha yao ya kiroho na kuendelea kuishi upendo, umoja na mshikamano unaofundishwa na Kristo.


Heri ya Sikukuu ya Ekaristi Takatifu kwa waamini wote.