




Na, Juventus Juvenary-Kabanga.
Kampuni ya RUKUNDOO Coffee Traders inayojihusisha na bidhaa ya Kahawa, imekabidhi kompyuta mpya tano kwa Shule ya Sekondari Kabanga, ikiwa ni sehemu ya mchango wa kampuni hiyo katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA na mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Kompyuta hizo zimekabidhiwa na Bw. Nuru Christopher Nzoya, kwa niaba ya Mkurugenzi mwenza wa Rukundoo Coffee Traders, Wilson Dan Nathanael, wakati wa Mahafali ya 34 ya Kidato cha Nne yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Kabanga.
Bw. Nuru Nzoya, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, amesema kompyuta hizo tano ni sehemu ya utekelezaji wa ombi la shule lililoomba jumla ya kompyuta 10 ili kupunguza changamoto ya uhaba wa vifaa vya TEHAMA.
Bw. Nuru Nzoya pia amekabidhi mipira kwajili ya michezo huku akisema Rukundoo Coffee Traders haitasimama na hatua hiyo pekee, bali itashirikiana na wadau wengine kuhakikisha kompyuta tano zilizobaki zinapatikana.
Katika hatua hiyo, amesema atashirikiana na Mbunge wa Jimbo la Ngara, Dotto Jasson Bahemu, pamoja na Diwani wa Kata ya Kabanga, Hafidh Abdallah, katika kutafuta kompyuta hizo tano ili kukamilisha idadi iliyoombwa na shule.
Awali, akisoma risala ya shule, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kabanga, Onesmo Beyanga, amezitaja changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo na zinazohitaji ushirikiano wa wadau, ikiwemo uhaba wa maji na vifaa vya michezo, sambamba na mahitaji mengine ya kuboresha mazingira ya elimu.
Mchango huo wa Rukundoo Coffee Traders umeongeza nguvu katika juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuwawezesha wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kabanga kupata fursa zaidi za kujifunza na kutumia teknolojia katika elimu yao.
