Madiwani wa Darasa la 7 Pumzikeni, Jamii Inahitaji Kundi Jipya la Kuiwakilisha 2025/2030 : Teknolojia na Utandawazi Vimesaliti Uwezo wenu

By Titho Philemon May 19, 2025

Ushauri Maalumu kwa Serikali na Vyama vya Siasa Nchini


Ndugu Wanangara, Wana Kagera, Viongozi wote wa Vyama vya Siasa na Serikali, ninawasalimia kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania….!

Baada ya Salamu hizo nitumie nafasi hii kutoa ushauri wangu Maalumu kwa Serikali na Vyama vya Siasa Nchini kuhusu KUKOMA kwa Uwakilishi wa Waheshimiwa Madiwani wenye Elimu ya Darasa la 7 katika uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba 2025.

Kwa Mujibu wa Sheria, Kifungu cha 59(1) na (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani No. 1 ya Mwaka 2024, kimeainisha sifa stahiki anazopaswa kuwa nazo Mgombea Udiwani huku sifa ya kujua kusoma na kuandika ikiwa sehemu ya sifa hizo bila kuainisha kiwango anzia cha elimu ili kuweza kugombea udiwani.

Kwa miaka mingi sasa Halmashauri zote za Tanzania zipatazo 184 zimekuwa zikipitia katika changamoto za kiutendaji na kiutawala kutokana na ufinyu wa hoja jenzi ndani ya mabaraza ya Madiwani katika halmashauri zetu huku chanzo kikiwa ni wingi wa Madiwani wa Darasa la 7 kuliko kawaida hali inayoifanya Halmashauri kulemewa na wakati mwingine kuongozwa na wataalamu (wageni waajiriwa) hali ambayo huondoa dhana nzima ya udiwani kama uwakilishi.

Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ni Moja kati ya Halmashauri za Tanzania zinazoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri mwenye Elimu ya Darasa la 7, kiasi kwamba kama kusingekuwa na Mkurugenzi wa Halmashauri (katibu wa Baraza la Madiwani) Mzalendo, Mchapakazi na mwenye kujali na kutii kiapo chake cha Utumishi ipasavyo huenda hata tusingejua miradi inaendaje na inasimamiwaje kwa umuhimu. Hili nalo linapaswa kutufikirisha.

Ni wakati sasa wa Serikali na Vyama vya Siasa kikiwemo chama tawala (CCM) kuja na Mbadala Mpya wa kuwezesha kundi jipya (Elimu ya Kidato cha 4 na zaidi) kuingia kwenye Mabaraza ya Madiwani katika Halmashauri zetu ili kuweza kuondoa mkwamo huu unaozikabili Halmashauri Nyingi Nchini. Vyama vya Siasa kuteua Watiania wa Udiwani wenye Darasa la 7 katika Karne hii ya Utandawazi (Sayansi na Teknolojia) ni kudumaza kwa maksudi fikra mpya za kijamii na kufunga mpenyo wa mawazo mapya katika Halmashauri zetu nchini.

Kwanini Madiwani wenye Elimu ya DARASA LA 7 Wawekwe Pembeni Uchaguzi Mkuu 2025?

  1. Mfumo wa Kidigitali na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia VIMESALITI fikra zao na uwezo wa uelewa wao wa mambo na hivyo kuaminiwa kwao tena kutaongeza mzigo katika Halmashauri zetu nchini.
  2. Uwezo mdogo katika kuchanganua na kujenga hoja kuhusu Miradi, Mikataba, Sheria ndogo ndogo na baadhi ya mambo ya msingi ndani ya Halmashauri.
  3. Kukosa SAUTI na Kujaa Woga kwa hofu ya Uchache wao wa Maarifa kwenye Baraza katika kuhoji masuala Mtambuka hasa pale kunapoonekana dosari katika miradi ya Maendeleo kwenye Halmashauri zao.
  4. Uwezo na ufanisi mdogo katika kubuni, kukagua, kusimamia na kutolea taarifa miradi ya maendeleo katika kata zao.
  5. Madiwani wenye Elimu ya Darasa la 7 wakiwa wengi sana Ndani ya Baraza la Madiwani la Halmashauri, Baraza la Madiwani hukosa Nguvu na Hivyo kuongozwa na Watumishi wa Halmashauri (kutokana na uchache wao wa maarifa) badala ya wao kuiongoza na kuisimamia halmashauri. Hii inauma sana na nia aibu kubwa sana kwa chama na serikali.
  6. Kupunguzwa kwa Watu wa Kundi hili kutarejesha thamani ya vyama vya siasa (kikiwemo Chama cha Mapinduzi – CCM) katika kukomaza Demokrasia na Kuongeza ushindani wenye tija miongoni mwa vyama vya siasa nchini.

Madiwani wenye Elimu ya Darasa la 7 walikuwa wanapatikanaje kwenye Halmashauri zetu ?

UHALSIA UKO HIVI :-
Wananchi zaidi ya 70% wa Ngara (kama eneo langu la utafiti) wanapenda viongozi wenye Maarifa mapana na ujuzi wa mambo kuwaongoza. Lakini kuna sababu kubwa Nne (4) zilizokuwa zinafanya hali inakuwa tofauti katika chaguzi na hivyo kusaliti utashi halsia wa wananchi, nazo ni :-

  1. _Uteuzi wa Dharura na wa Kimkakati kwa maeneo yaliyokuwa yakitengwa kuwa kata mpya;- Kwa mujibu wa utafiti wangu, nilibaini kuwa wenyeviti wa vijiji wengi wenye Elimu ya Darasa la 7 walikuwa wakiteuliwa kwa maelekezo ya chama (kama wanavyodai) na kwenda kugombea udiwani pale inapotengwa kata mpya na hivyo kwenda kuwa madiwani, bila kujali uwezo wao na upana wao kifikra.
  2. Mifumo mibovu ya Uteuzi ndani ya Vyama vya Siasa ;- Makatibu wa vyama hususani Chama cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wakiengua form za wagombea udiwani (na wengine kupoteza fomu za wagombea wale ambao hawana maslahi nao) na hivyo kupelekea kupatikana kwa wagombea wa Darasa la Saba kutokana na maslahi ya viongozi wachache wa chama ndani ya Kata na kuponza maamuzi ya jamii nzima. Kuna majina yalikuwa yanaenguliwa yanarudi majina ya wale ambao ni chaguo la chama na siyo chaguo la wananchi (hali ambayo ilikuwa ikikatisha tamaa na kuamua kumpigia kura yoyote) na kama mjuavyo mpinzani kupenya ilikuwa ni mbinde na hivyo kujikuta kata inapata diwani wa CCM wa darasa la 7.
  3. Rushwa ya Ngono ;-, wapo madiwani wengi hususani wale wa Viti Maalumu Kundi la Wanawake (wenye Elimu ya Darasa la 7) ambao walikuwa wanapenyezwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kwa rushwa ya Ngono na hivyo kupelekea kuongezeka kwa mzigo mzito katika halmashauri zetu ndani ya Ngara, Kagera na Taifa kwa ujumla.
  4. Vitisho vya Watia Nia dhidi ya Wagombea Wenza ;- Hii ilikuwa ni mifumo ya Kidikteta ndani ya vyama vya siasa hususani chama tawala ambapo Diwani mtiania alikuwa anathubutu kutishia kwa maneno kumdhuru mgombea mweza katika udiwani endapo tu atachukua fomu na hivyo kupelekea hofu na mashaka na kususia kugombea kwa baadhi ya watia nia. Matokeo yake hii imepelekea jamii kupata (i) Madiwani wa Darasa la 7 wengi katika Mabaraza ya Madiwani kwenye Halmashauri zetu (nyingi) nchini ikiwemo Halmashauri ya Ngara, (ii) Madiwani wengi kuongoza Mihura Minne hadi Mitano (Miaka 20 hadi 25) ya udiwani katika kata zao, (iii) Kata nyingi kutoendelea kutokana na utawala wa kimazoea, (iv) Halmashauri nyingi kukosa ubunifu mpya na fikra mpya na hivyo kuwapa mzigo wateule wa Rais (Wakurugenzi) pamoja na Watumishi walioajiriwa katika Halmashauri husika.

Kama Sifa ni Kusoma na Kuandika na hakuna kigezo cha Elimu katika Katiba na Sheria ya Uchaguzi nchini, chama na Serikali vifanye nini ili Kufanikisha hili la Kuengua Madiwani wenye Elimu ya Darasa la Saba uchaguzi Mkuu 2025 ?

ILI KULINDA MASLAHI MAPANA YA JAMII, na bila kukiuka sheria za nchi na katiba ya nchi chama na Serikali vinapaswa kufanya yafuatayo ;-

  1. Vya siasa vihakikishe vinateua Wagombea wenye Sifa ambazo kwao wataamini kuwa mtu huyo anaweza kuchangia ujenzi wa jamii mpya kifikra na kimtazamo bila kujali elimu yake.
  2. Kila Chama cha Siasa kwa ngazi ya kata kitoe nafasi ya wazi kwa wagombea wote (kwa wakati maalumu) kusimama mbele ya uongozi wa chama na wajumbe (wapiga kura wanachama) kunadi sera zao kisha kupitia sera hizo za uwazi chama kipendekeze majina matatu kati ya wote na kisha kiyakabidhi kwa wapiga kura kwaajili ya kushindanishwa na kupigiwa kura kumpata mmoja. Hiyo itakuwa njema sana.
  3. Ubunifu wa miradi mipya katika kata na Vikao vya Mheshimiwa Diwani viwe ndo vigezo kikuu vya kumfanya diwani aliyepo madarakani kuteuliwa kati ya majina matatu kwaajili ya kuwania muhula mwingine. Hii itainua hadhi ya chama cha siasa na kukiimarisha zaidi.
  4. Vitendo vya Rushwa ikiwemo Rushwa ya Ngono vidhibitiwe katika michakato yote ya Uteuzi ili kuweza kupata Wagombea Safi wenye Karba njema na wenye uwezo wa kukiwakilisha vema chama na serikali katika maeneo yao ya utawala (katani kwao).
  5. Baada ya uteuzi wa majina matatu kutoka uongozi mkuu wa chama, kura halali za wanachama (wajumbe) ziheshimiwe katika kutoa maamuzi ya nani ni mshindi na aliyeaminiwa katika kinyang’anyiro hicho.

Kwa Mfumo huo, na kwa namna nyingine yoyote bora ambayo VYAMA VYA SIASA (kikiwemo Chama cha Mapinduzi – CCM) na serikali vitaona inafaa TUNAWEZA kupunguza uwakilishi wa Madiwani wa darasa la Saba na hatimaye kuongeza uwakilishi imara, madhubuti na bora katika Halmashauri zetu nchini.

Kazi na Utu, Tunasonga Mbele Pamoja!

Asanteni sana🤝🙏

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *