Waajiri wa Wachunga Ng’ombe (W) Ngara Wajalini Wafanyakazi Wenu

By Titho Philemon May 20, 2025

Ushauri Maalumu kwa Umoja wa Wafugaji (W) Ngara


Naanza andiko langu kwa Kunukuu Kauli ya Mmoja wa Wachunga Ng’ombe wilayani Ngara (Jina lake Kapuni)

“…Kaka Titho, kwakweli hii kazi ya KUCHUNGA NG’OMBE ni ngumu sana, yaani Mvua ni Yetu, Jua ni Letu, Baridi ni Letu aliko Umushahara nubhusa, Laki mbili na Nusu Gusa kumwaka nahonyene kuuronka nukwitonda. ….” (Mwisho wa Kunukuu.)

Mkoa wa Kagera unakadiriwa kuwa na Ng’ombe wapatao 554,380 wanaofugwa huku Ng’ombe wa Asili wakiwa 534,299 na Ng’ombe wa Maziwa wakiwa 20,081. Kati ya Ng’ombe wote hao, Ng’ombe wapatao 513,832 sawa na 92.7% wanapatikana maeneo ya Vijijini { Chanzo : Tovuti ya Mkoa wa Kagera}

Kutokana na Takwimu ya Kimkoa hapo juu ni dhahiri kuwa Maeneo ya Vijijini yakiwemo maeneo yetu ya Ngara ndiko kunakopatikana mifugo mingi (Ng’ombe).

Imekuwa ni desturi ya muda mrefu kuwa wafugaji wengi wa Ngara huwa hawachungi mifugo yao wenyewe na badala yake huwaajiri wachungaji na kuwalipa kwa mwezi, kwa Mwaka au kwa kuwapa Ng’ombe kadri ya makubaliano yao.

Pamoja na kazi ya KUCHUNGA NG’OMBE ambayo wanakuwa wameajiriwa kuifanya vijana hao (wachungaji) hufanyishwa kazi za ziada kama vile ;-

  1. Kulinda Mifugo Usiku dhidi ya Wavamizi, Wezi pamoja na kuwadhibiti Ng’ombe wasitoroke Usiku kwenda kuharibu mashamba ya watu.
  2. Kutibu Mifugo wao wenyewe au kwa kushirikiana na Maafisa Mifugo (kutokana na matakwa ya Mwajiri wao)
  3. Kuhesabu idadi ya Ng’ombe asubuhi kabla ya kutawanyika kwenda malishoni na Usiku baada ya kutoka Malishoni
  4. Kukamua Maziwa kila siku asubuhi kabla hajapeleka Ng’ombe malishoni na usiku baada ya kuwatoa malishoni.
  5. Kufuata chakula kwa Mwajiri (umbali Mrefu), kusafirisha chumvi (kwa wale ambao hawaletewi chumvi na waajiri wao) pamoja na wengine kushiriki kazi za nyumbani kwa Mwajiri hususani pale anapokuwa amepumzika (kwa yale mazizi / Makundi yenye mchungaji zaidi ya Mmoja)

PAMOJA NA MAJUKUMU YOTE HAYO wanayoyafanya hawa Vijana Wachunga Ng’ombe lakini bado mishahara yao kwa mwaka HAIRIDHISHI!

Kijana analipwa Tshs 250,000/= kwa Mwaka sawa na Tshs 20,833/= kwa Mwezi. Wapo wale wanaolipwa Tshs 300,000/= kwa Mwaka sawa na Tsh 25,000/= kwa mwezi. Lakini vilevile ninatambua kuwa wapo wanaolipwa kiwango mseto kwa mkataba wa miezi 9 hadi 10 (aidha Tsh 300,000/=) kwa miezi 10 sawa na Tsh 30,000/= kwa mwezi, bila kusahau wale wanaolipwa kwa kupewa Ng’ombe baada ya muda kadhaa.

Kutokana na sababu kama ;-

  1. Mabadiliko ya Tabia ya Nchi,
  2. Sababu ya Kijiografia kwa maeneo mengi ya Ngara,
  3. Umbali uliopo katika kuyafuata maeneo ya Malisho na Manywesho,
  4. Hali ya Mvua Kali (yenye upepo, radi, na yenye kuwasababishia homa zisizoelezeka)
  5. Hali ya Jua kali hususani msimu wa kiangazi wanapokuwa wanahangaika kusafiri umbali mrefu kutafuta maji na maeneo bora kwa malisho
  6. Hali hatarishi ya Ulinzi wa Mifugo Usiku pamoja na shughuli nyinginezo hatarishi zinazoweza kutokea katika mlengo huo (ikiwemo kushambuliwa au kuumizwa na Ng’ombe wakorofi),

Ni wazi na inanipendeza kusema kuwa MSHAHARA WAO NI MDOGO SANA ikilinganishwa na shughuli nzito, hatarishi, ngumu na ya uvumilivu wanayoifanya tena wengine wakiwa ni vijana wadogo wenye ndoto na malengo makubwa ya kufanikiwa maishani. Hili suala linaumiza sana!

BINAFSI ili kurejesha hali ya Ujira wa Haki kwa VIJANA WACHUNGA NG’OMBE hapa wilayani Ngara ninapendekeza na kushauri yafanyike mambo yafuatayo : –

  1. Uongozi wa Umoja wa Wafugaji (W) Ngara (kama upo) uitishe kikao cha dharura cha wafugaji wote ili kuweza kujadili suala la nyongeza ya Stahiki zao (Mshahara) kulingana na maeneo au katika uchambuzi ule watakaouona unafaa.
  2. Maazimio ya Kikao cha Umoja wa Wafugaji (W) Ngara yaje na kima cha chini cha mshahara (Minimum Salary Scale) ambacho kitakuwa kima cha chini na cha mwisho kabisa kwa Mchunga Ng’ombe anayechunga katika mazingira mazuri na rafiki.
  3. Kumekuwa na Tabia ya Wafugaji kuajiri wafanyakazi (Wachunga Ng’ombe) ambao siyo Raia wa Tanzania na wengine hawapajui kwao. Hii ni hali ya hatari sana kiusalama hususani dhidi ya wafugaji wenza pale kunapokuwa na migogoro dhidi ya wachungaji wa Makundi tofauti, au wao kwa wao. Waajiri wasimamie sheria na umoja wa wafugaji uratibu hilo.
  4. Ili kuhakikisha Vijana wachunga Ng’ombe wanalipwa stahiki zao ipasavyo, kupitia aidha umoja wa wafugaji wa wilaya au Mamlaka za Kiutawala za Wilaya waajiriwa wote (wachunga ng’ombe) wawe na Register maalumu kwa viongozi wa mtaa, vitongoji, vijiji hadi kata kwaajili ya utambuzi ikiwa ni pamoja na suala la usalama wao binafsi sambamba na usaidizi pale watakapokuwa na shida za kiraia kutoka kwenye ofisi husika (mamlaka za mitaa).
  5. Uwekwe utaratibu wa kwamba mikataba yote ya Wachungaji kuajiriwa kazini (kuanza kuchunga) isainiwe mbele ya Mamlaka za kiserikali (Viongozi wa Mitaa, vijiji n.k)
  6. Mikataba baina ya Mwajiri na Mwajiriwa (Kijana Mchunga Ng’ombe pale inapotaka kuvunjwa uvunjifu huo wa mkabata ufanyike mbele ya uongozi hususani mbele ya mamlaka zilizosaini mkataba huo kipindi mwajiriwa anaanza kazi (Sababu za Kuvunjika ziainishwe)
  7. Mishahara ya VIJANA WACHUNGA NG’OMBE ianzie angalau TSH 50,000/= kwa mwezi kwa wenye kima cha chini kabisa cha Mshahara.
  8. PALE ITAKAPOBIDI mamlaka za Kiutawala za kiwilaya hususani Ngara, ziingilie kati ili kuhakikisha vijana wanaoajiriwa kuchunga Ng’ombe wanalipwa mishahara kutokana na uzito wa kazi zao (ujira unaowastahili) kama lilivyotakwa na haki ya kikatiba kwa mujibu wa Katiba ya Nchi yetu ya Mwaka 1977.

Mwisho : Leo nimejikuta nimelikumbuka kundi hili kama kundi la Msingi ambalo limesahaulika sana katika jamii.

Mungu wabariki Vijana Wachunga Ng’ombe Ngara!
Mungu Ibariki Ngara!
Mungu Ibariki Tanzania!

Kazi na Utu, Tunasonga Mbele Pamoja!🇹🇿🇹🇿🙏

Leave a Reply