AHADI YA WAZIRI WA NISHATI YATEKELEZWA NDANI YA SIKU 9

By Na Mwandishi May 18, 2026

Ikiwa ni siku tisa tu tangu Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi kufanya ziara Wilayani Ngara, Serikali imetekeleza ahadi yake ya kutatua changamoto ya umeme kwa kupeleka Transfoma kubwa yenye uwezo wa MVA 10.

Leo Jumatatu Mei 18, Transfoma hiyo imewasili na kuanza kufungwa katika eneo la Djuruligwa kwa lengo la kupunguza tatizo la kukatika kwa umeme ambalo limekuwa likikwamisha shughuli za maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Ngara.

Wakati wa ziara ya Waziri huyo, alipoweka jiwe la msingi katika mradi wa kusafirisha umeme kutoka Benako-Ngara kwenda Kyaka, Mbunge wa Jimbo la Ngara Dotto Jasson Bahemu aliwasilisha kero ya kukatika mara kwa mara kwa umeme na kuomba suluhisho la kudumu.

Baada ya kupokea maombi hayo, Waziri Ndejembi alitoa maagizo ya kutafutwa kwa Transfoma kubwa yenye uwezo wa kuimarisha huduma ya umeme Wilayani Ngara.

Hatimaye leo, wananchi wameanza kushuhudia utekelezaji wa ahadi hiyo kwa vitendo ambapo Transfoma hiyo inaendelea kufungwa chini ya usimamizi wa maafisa wa TANESCO Ngara wakiongozwa na Mhandisi Amani Chidundo.

Pichani ni Katibu wa Mbunge, Soud Mkubila, Katibu Msaidizi Juventus Juvenary pamoja na maafisa wa TANESCO Ngara wakifuatilia hatua kwa hatua zoezi la ufungaji wa Transfoma hiyo.