BAHEMU AUNGA MKONO POLISI JAMII CUP, ATOA VIFAA VYA MICHEZO NGARA

By Na Mwandishi Jul 3, 2026

Na, Juventus Juvenary-Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ngara.

Leo, Julai 3, 2026 – Mbunge wa Jimbo la Ngara, Mheshimiwa Dotto Jasson Bahemu, leo ameshiriki uzinduzi wa mashindano ya Polisi Jamii Cup kwa kukabidhi vifaa vya michezo kwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Ngara.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mipira na filimbi (vipenga), vitakavyotumika katika mashindano yatakayofanyika katika kata zote za Wilaya ya Ngara, yakilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi kupitia michezo.

Akizungumza katika hafla hiyo mbele ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Blasius Chatanda, Mheshimiwa Bahemu amesema ataendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, ameahidi kuongeza nguvu katika mashindano hayo kwa kuchangia mipira zaidi na zawadi mbalimbali kwa timu zitakazoshiriki, hatua inayotarajiwa kuongeza hamasa, kukuza vipaji vya vijana na kuimarisha uhusiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi.

Mashindano ya Polisi Jamii Cup ni sehemu ya jitihada za Jeshi la Polisi za kuimarisha ushirikiano na jamii, kuhamasisha amani, usalama na mshikamano kupitia michezo.