HISTORIA YA JINA LA WAHANGAZA
Nianze kutoa shukurani za dhati kwa Mjoli wa Historia na diplomasia ya ulimwengu Comred Mbwana Allyamtu. Makala hii kwa asilimia nyingi inatokana na andiko lake la 19/11/2019.
Wahangaza ni kabila moja kati ya mawili (Washubi na Wahangaza) wanaopatikana Wilayani Ngara katika Mkoa wa Kagera.
Wilaya ya Ngara ni wilaya inayopatikana Mkoa wa Kagera kaskazini magharibi mwa Tanzania. Inapakana na nchi za Rwanda na Burundi na lugha ya Wahangaza na Washubi ni kihangaza na kishubi ambapo lugha hizo zinaingiliana kwa karibu 92% na lugha za nchi ya Rwanda na Burundi hali inayorahisisha mawasiliano na raia wa mataifa hayo jirani.
Njia kuu za kuingia nchi za Rwanda na Burundi zinapatikana ndani ya wilaya ya Ngara, ambapo kwa Burundi hutumia mpaka wa Kabanga/Kobero kuingia Burundi, mpaka huu unachangia 2.9% ya pato la taifa huku ukitoa 6.2% ya export index ya bidhaa zote za Tanzania zinazotoka nje, kwa upande wa mpaka wa Tanzania na Rwanda mpaka unaotumika ni mpaka wa Rusumo, huu mpaka uchangia 7.1% ya pato la taifa huku export index ikichangia 17.96% ya bidhaa zote za Tanzania zinazotoka nje.
Jina la asili la wilaya ya Ngara kabla ya kuitwa Ngara iliitwa Kibimba (yaani pori). Chanzo cha jina hilo la Ngara lilitokana na sehemu iliyokuwa maalumu kwa mikutanao ambayo ilifanyika chini ya miti mikubwa inayoitwa iminyinya yingara( ilikuwa miti mikubwa yenye matawi yaliyosambaa) ambapo kwa sasa eneo hilo ndipo ilipo halmashauri ya wilaya ya Ngara pale eneo la junction na mti wa kumbukumbu upo mpaka sasa pale ndani ya majengo ya halmashauri ya wilaya ya Ngara, Mti huo wa Umunyinya uliopandwa Halmashauri ya wilaya ya Ngara ambao asili yake imebeba jina la Ngara.
Wilaya ya Ngara ilikuwa na watawala wa kichifu ambapo kulikuwa na machifu wa pande mbili yaani chifu wa Bugufi na Chifu wa Bushubi. Machifu waliotawala Bugufi walikuwa Balamba wa kwanza, Rusengo, Ruvubi, Mpanda, Kanyamazinge na Balamba motto waKayamazinge. Machifu hao wa Bugufi na Bushubi walikuwa wakikutana eneo la Nyamilama ili kupeana maadili na mbinu za kiutawala mfano lilivyo bunge la Dodoma kwa sasa. Na Bushubi alikuwepo chifu Nsoro.
Dola ya Bugufi ilikuwa ikipatikana katika bonde lote la Bugufi linaloanzia kaskazini magharibi mpaka kusini mashariki na wafalme wa Bugufi kuanzia Baramba I mpaka kwa Baramba mtoto wa
Kinyamazinge walitawala eneo la dola ya Bugufi ambayo makao makuu ya dola hiyo ilikuwa pale Kanazi, Mfalme wa kwanza wa Bugufi alikuwa ni Baramba I aliyeingia Ngara miaka ya 1680 akitokea Rwanda pamoja na wafanyakazi wake ( Abagaragu). Kwa asili alikuwa akitokea kwenye ukoo wa kifalme wa Ankole huko Uganda ulikuwa unaitwa wahinda (royal bahinda clan of Ankole ). Huu ni ukoo ulioibuka baada ya kumeguka kwa ukoo mkubwa wa kifalme wa Wanyiginya kutokana na ndugu wa damu moja kunyang’anyana maeneo ya kutawala ndani ya eneo la maziwa makuu( Great lakes region), huu ukoo wa Wanyanginya nao ulifika eneo la Ankole miaka ya 1297 ukitokea Axum huko Ethiopia.
Kama ilivyo kwa wafalme wengine wa ukoo wa Wahinda alikuwa ni Muhima na alioa wake zake kutoka kwenye jamii za wahima( watutsi). Aliingia Rusumo na kuweka makazi yake katika Mlima Shunga na kuwa mfalme wa kwanza wa Ngara. Mfalme Baramba I alikuwa na watoto wakubwa wawili ambao waliitwa Mpumirizi na Mpanda na Mpumirizi ndo alikuwa mzaliwa wa kwanza na ndiye alitakiwa awe mfalme lakini haikuwa hivyo, kuna makosa yalifanyika mdogo mtu mpanda akawa mfalme badala ya kaka yake (hii ntakuja kulieleza siku moja). Orodha ya wafalme wa Bugufi ni Baramba I, Mpanda, Ruvubi, Rusibana, Rusengo( mdogo wake na Rusibana baada ya Rusibana kufariki vitani kwenye vita kati ya Warundi na Wahangaza), Kinyamazinge( Son of Rusengo) na Baramba II pia walikuwepo mpanda II na Ruvubi II ila walikuwa kama ceremonial chiefs tu kwa sababu uchifu wa madaraka uliishia kwa Baramba II.
Mila na desturi ya wahangaza na washubi, zinafanana kwa kila kitu, katika mila zao mtoto alikuwa haruhusiwa kukaria kiti cha baba yake wala kula sahani moja na wazazi wake hivyo walitengwa pembeni na kula peke yao, Wahangaza walikuwa hawaruhusiwi kula kondoo na mbuzi bali kondoo na mbuzi waliliwa na kabila duni lijulikanalo kama watwa ambao hawa Watwa ni kabila la asili huko milima ya Urundi (Burundi ya Sasa), hawa Watwa walikuwa ni watumwa na wajakazi wa wahangaza na washubi, ( mbuzi aliitwa impene kwa sababu waliichukulia kama ipo uchi na ndio sababu ya kutoliwa na kabila hilo enzi hizo.
Imani ya wahangaza na washubi (Dini) ilikuwa ni kuabudu chini ya miti ya Milumba (Ibivumu) waliabudu Mungu aliyeitwa Kiranga kilumwelu (Mungu wa amani) na pia kutambikia kwenye vijumba vidogo vilivyoitwa Indaro,na waliamini katika tiba za asili.
Msichana akibeba mimba nje ya ndoa ya kimila adhabu yake ilikuwa ni kufungwa jiwe la kusagia na kutupwa mto Ruvubu eneo lililojulikana kama Mmasangano (Nyaburumbi), na adhabu nyingine ilikuwa ni kumfungia sagio (jiwe la kusaga) na kuwekwa njiapanda (amayilabili) ili aliwe na wanyama mpaka kufa, mabinti wengi waliogopa adhabu hizo hivyo walitii mila na desturi. Wahangaza walitumia tiba ya asili yaani miti shamba kwa magonjwa, pia kuondoa mizimu iliyokuwa inawasumbua watu alikuwa anatafutwa mbuzi au kuku mweupe wa kafara na mgonjwa kuruka kafara hiyo kisha kutupwa porini kwenye miti iitwayo imilinzi.
Utamaduni wa kuoana ilikuwa ni kwamba kijana hakuruhusiwa kutafuta mchumba bali wazazi wake walimchagulia mchumba kwa kuangalia historia ya ukoo au familia anakotoka mchumba husika. Wazazi wa pande zote mbili walikubaliana kwa kupeana mahari (posa) ya jembe la mkia (jembe la asili) au nguo zilizotengenezwa kutokana na magome ya miti (ikibugu). Binti alipelekwa usiku kuolewa.
Mahusiano ya watu yalidumishwa kwa kutembeleana baada ya kuandaa pombe ya asili yaani “impeke na gwagwa”. Kulikuwa na aina mbili ya unywaji wa pombe hii, aina ya kwanza watu walialikwa na kujumuika sehemu moja walipoitwa na familia iliyoandaa pombe hiyo hasa hasa msimu wa mavuno (kiangazi) illiitwa “gutumila” na pia njia nyingine ilikuwa ya kwenda na mitungi ya pombe kutembelea familia Fulani( kugemura). Wanawake na watoto walizuiliwa kunywa aina za pombe isipokuwa walikunywa pombe ya ndimasi au iliyochakachuliwa (umusharulo).Burudani ya kabila hizo ni na ngoma ya asili ya wahangaza ilikuwa ikiitwa “imyiyereko” yaani ngoma ya asili ambayo ilichezwa kwa madaha huku wakiruka juu.
Shughuli kuu ya kabila hili ilikuwa kilimo, ufugaji kwa kiasi na uwindaji wa wanyama, watoto walirithishwa mila na wazazi wao kwa kupewa elimu ya vitendo na hasa kugawa kazi kwa kuzingatia mgawanyiko wa kazi kijinsia.
Historia ya jina “Hangaza” kwa mujibu wa historia ya mababu zetu inatokana na neno la kirundi/kinyarwanda la “Hangaaza neza ulibe yo bali” yaani “angalia kwa makini uone walipo” historia ya maneno haya yalitoka kipindi cha vita kati ya dola ya Bugufi na dola za Urundi na Uruanda.
Kwa mujibu wa simulizi za babu zetu ni kwamba hapo zamani kulikuwa na watemi wawili wa nchi mbili tofauti yaani Burundi na Rwanda kwa sasa , watemi hao walikuwa mtemi Mwambutsa wa Burundi na mtemi Kigeri wa Rwanda ambao waliamua kuunganisha nguvu ili kuvamia dola ya Bugufi, watemi hao wawili walikuja kupigana na mtemi Kinyamazinge wa Ngara, watu wa Ngara walibuni vita ya kupigania mpakani (boarder defensive) ambapo mababu zeetu walishinda mchana kutwa wakikata miti na usiku ambao ndo ulikuwa muda wa vita walikoka moto mkubwa, sasa wale warundi na wanyarwanda walipokuja kupigana vita vya ana kwa ana( full force attack) walishangaa kuona moto mkubwa ukiwaka wakati muda huo wapiganaji wa Ngara yaani mababu zetu wakiwa tazama vizuri na kuwapiga mishale kwa urahisi sababu ya mwanga wa moto ndipo neno “Hangaaza” lilipo zaliwa likiwa na maana ya tazama kwa umakini kwa lugha ya Kiswahili.
Neno hilo lilianzia pale maana warundi na wanyarwanda hawakuweza kuwaona vizuri wapiganaji wetu maana walikuwa kando kidogo na moto huo hivyo wakawa wanaambiza “hangaaza neza ulibe yo bali” yaani “angalia kwa makini uone walipo” (kwa kiswahili). Na pia kipindi hicho lilitumika zaidi kumaanisha mwanga wa vita kuanzia hapo wenzetu wa Burundi na Rwanda baada ya kushindwa vita hiyo ndipo walipoanza kutuita wahangaza (yani walio weza kuona), na ndipo msemo wa kilugha unasema “Utazi umhangaza amuhanga amaso” ulipoanzia.
Toka hapo jina “Hangaza” lilianza kutumika kuwatambulisha kabila la wahangaza, wahangaza ni kabila la watu wakalimu sana, wenye upendo na roho za kujali wageni, chakula kikubwa katika wilaya ya Ngara ni ndizi, mahargwe na mihogo, pia hulima mazao ya kahawa toka mwaka 1950 huku pia miaka ya Karibu wengi wa wakulima wameanza kulima maparachichi (avocado), pia shughuri za uvuvi hufanyika katika mto Ruvubu (Ruvuvu).
Ikiwa una nyongez juu ya makala au maoni tafadhali tuandikie.

