MAKALA MAALUMU NA JOSIAS CHARLES

By Benny Bert Apr 18, 2025

Mwandishi wetu amefanya mahojiano maalumu na Josias Charles, moja ya wanasiasa Vijana kutoka Jimbo la Ngara ambaye siku za hivi karibuni alizua gumzo baada ya kuonyesha kutafakari kuhusu maombi ya wananchi wenzake wa Jimbo la Ngara kumtaka agombee nafasi ya Ubunge wa Jimbo hilo.

Ndugu Josias Charles

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwa njia ya Simu na ndugu Josias Charles yalilenga kujua msimamo wake haswa ni upi kuhusu tetesi kuwa ana mpango wa Kugombea nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Ngara. Lakini pia mazungumzo yetu yalilenga kufahamu baadhi ya mambo kuhusu maisha yake binafsi. Hapa chini nimekuandalia Makala fupi kuhusu mwanasiasa huyu kijana ambaye ni machachali kweli kweli.

Mwandishi: Ni kweli una mpango wa Kugombea Ubunge wa Jimbo la Ngara?

Josias Charles: Ni mapema sana kusema kuwa nitagombea ama la, lakini kugombea ni chaguo bora zaidi kwani Ngara bado inahitaji mchango wa Vijana wenye sifa, uwezo, ujasiri na ari ya kuwatumikia katika kutafuta majibu ya kero za msingi kama vile kudai haki za wananchi ambao wamekuwa wakisumbuliwa kwenye suala la Fidia, Kushughulikia changamoto ya wananchi kunyanyaswa kwa kigezo cha uraia wanapodai haki zao, kushughulikia changamoto ya Ajira na uwezeshaji kwa Vijana na akina mama na mengine mengi.

Mwandishi: Watu wengi wanatamani kukufahamu kwa undani, asili yako haswa ni eneo gani la Wilaya ya Ngara?

Josias Charles: Okay, Mimi ni Mtoto wa pili katika familia ya watoto watano wa Mzee Charles Isaya Rutuma nimezaliwa kata ya Ngara Mjini, Kijiji cha Mubinyange ambako wazazi wangu wameishi toka mwaka 1990. Mimi na ndugu zangu wote tumezaliwa na kuishi hapo kwa kipindi chote cha maisha yetu. Asili ya Baba yangu ni kijiji cha Muhweza kilichopo kata ya Mabawe kitongoji cha Kukatongo kutoka familia ya Mzee Isaya Rutuma. Mama yangu Bi. Evelina Ndabise ni Mzaliwa wa Kijiji cha Mukididili kilichopo kata ya Ngara Mjini.

Mwandishi: Kwa miaka mingi umekuwa ukitumiwa na wanasiasa wengi wa Ngara katika Shughuli zao za kisiasa. Unadhani ni kwa nini umekuwa ukitumiwa sana na wana siasa?

Josias Charles: Nianze kwa kukurekebisha kidogo kauli yako kuwa sio kweli kwamba nimekuwa nikitumiwa na Wanasiasa kwenye shughuli zao bali nimekuwa nikisaidiana nao ama nikishiriki shughuli mbalimbali za kisiasa kwa Utashi wangu. Nitakupa mfano, Mwaka 2015 nilikuwa moja ya watu wa karibu na walioshiriki kwenye Kampeni za ndani ya Chama wakati Dr. Philemon Sengati akiwania kuteuliwa kuwania ubunge wa Jimbo la Ngara. Baada ya mchakato ule nilihamia kwenye Team ya Mtandaoni ya Kampeni ya Rais Dr. John Pombe Magufuli. Baada ya Uchaguzi ule, mwaka 2016 hadi mwaka 2019 nilikuwa katibu wa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kagera, Mh. Oliver Daniel Semuguruka. Mwaka 2020 nilishiriki kumuunga mkono Hilali Ruhundwa ambaye alikuwa moja ya Vijana waliowania kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi kuwania ubunge wa Jimbo la Ngara. Bada ya hapo nimeshiriki katika baadhi ya Shughuli za Mbunge wa Jimbo la Ngara Mh. Ndaisaba Ruhoro mpaka pale mwaka 2024 nilipoamua kujiweka kando kutokana na ratiba zangu kuwa ngumu kutokana na kuanza masomo yangu ya Uzamili (Masters).

Mwandishi: Mara kadhaa umekuwa ukiibua utata kwa hoja zako zinazoonekana kutetea maslahi ya watu huku ukiwabana baadhi ya Viongozi wa Serikali. Hauoni kuwa jambo hili litakupa wakati mgumu kupata uungwaji mkono wa Viongozi hao?

Josias Charles: Hahahaha … Kwanza mpaka sasa sijaweka wazi kuwa nitagombea ama sitagombea. Lakini hata nikigombea nafasi yoyote sidhani kama kuna kiongozi atakuwa na kinyongo ama wasiwasi wa kuniunga mkono maana kwangu binafsi ninaamini viongozi wote wapo kusimamia maslahi ya Wananchi. Kwa maana hiyo ninapoibua changamoto na kuzipigia kelele ninaamini ninasaidia viongozi hao kuweza kuwahudumia wananchi vizuri zaidi. Binafsi ninajitahidi kuibua kero zinazogusa maisha ya watu bila chuki ama uonevu hivyo nina hakika kiongozi yoyote mzalendo anafurahishwa na namna ninavyoshughulika na mambo ya wana Ngara wenzangu hususani kupitia mijadala mizito kwenye mitandao ya kijamii.

Mwandishi: Nilipenda kufahamu kama umewahi kuwa kiongozi katika ngazi yoyote ama uzoefu wako kwenye masuala ya Siasa

Josias Charles: Mimi ni kiongozi katika level mbalimbali ambazo nimekuwa nikipita kuanzia Shule ya Misingi mpaka Chuo Kikuu. Mfano, nikiwa Chuo Kikuu cha Dodoma nilikuwa Mbunge wa Serikali ya Wanafunzi kutoka Kitivo cha Elimu (COED), nikawa Waziri wa Katiba na Sheria na baadaye nikawa Katibu Mkuu wa Serikali ya Shirikisho ya Serikali ya Wanafunzi wa Chuo kikuu cha Dodoma nikiongoza takribani wanafunzi 30,000. Pia mimi niliteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Vijana mwaka 2016 na baadaye kuwa Waziri Mkuu wa Bunge la Vijana la mwaka 2016. Wakati huo huo nilikuwa Mjumbe wa Shirikisho la Viongozi wa Serikali za Wanafunzi Tanzania (TAHLISO). Mwaka 2017 nilijitosa kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM Taifa japo sikufanikiwa kuteuliwa kugombea nafasi hiyo na chama changu CCM. Mwaka 2020 kwa awamu yapili nilikuwa sehemu ya Team ya Kampeni ya Mtandaoni ya Rais Dr. John Pombe Magufuli. Kwa ujumla nina historia kubwa kwenye masuala ya Uongozi na nimekuwa mtu ambaye ninarekodi nzuri ya kupigania haki na kuleta majawabu ya kero za wale ninaowaongoza.

Mwandishi: Katika mfumo wa siasa ambao rushwa ina mchango mkubwa katika kuamua nani awe kiongozi na nani asiwe kiongozi, unahisi una nafasi yoyote ya kuibuka na ushindi hususani kwa nafasi kubwa kama Ubunge?

Josias Charles: Ni kweli kuwa kwa sasa kumekuwa na tatizo kubwa ambalo limeifanya siasa kuwa kama biashara. Viongozi wa Chama cha Mapinduzi wamekuwa mstari wa mbele kukemea Rushwa na kutunga kanuni zinazowabana watoa rushwa. Pamoja na jitihada hizo, Mimi kama kijana ninaamini kuwa Jamii ikipata elimu kuhusu madhara ya Rushwa tunaweza kupata viongozi wazuri. Kuhusu kuwa na nafasi ya kushinda katika mazingira ya Rushwa hili siwezi kulizungumzia kwa sasa kwani bado sijafanya maamuzi ya kugombea. Kama nitafanya maamuzi hayo ninasema Tutavuka Daraja tukilifikia.

Itaendelea toleo lijalo……………….

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *