Ngara, Kagera – Juni 2025
Bw. Juventus Juvenary Illambona, aliyekuwa mwandishi wa habari wa Simamia TV na vyombo vingine mbalimbali ndani na nje ya nchi, ametangaza kuingia kwenye siasa kwa kuwania nafasi ya Udiwani wa Kata ya Kibimba, wilayani Ngara, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akiwa maarufu kwa jina la Juveilla, Bw. Illambona amesema amefanya tafakari ya kina kabla ya kuchukua uamuzi huo, kwa lengo la kuwatumikia wananchi wa Kibimba na kuleta mabadiliko chanya kwa kutumia uzoefu wake katika mawasiliano, usimamizi na utetezi wa maslahi ya jamii.

Vipaumbele Vyake Vikuu:
Miundombinu ya barabara, umeme na maji.
Kuhakikisha ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi ya baraza la madiwani.
Uongozi wa uwazi na utawala bora, kinyume na anachodai kuwa ni “uongozi wa kimazoea” wa Diwani aliyepo sasa.
Uwezeshaji wa makundi maalum: vijana, wanawake na walemavu kupitia mikopo na miradi ya maendeleo.
Maendeleo ya michezo, burudani na sanaa kwa kuanzisha matamasha ya kijamii.
Matumizi bora ya rasilimali zilizopo, hasa maji ya mto Ruvubu na uwanja wa ndege wa Ruganzo kwa ajili ya uchumi wa kata na wilaya.
Amesema iwapo atapata ridhaa ya wananchi, ataweka mfumo rasmi wa ofisi ya diwani kwa kununua kompyuta maalum kwa ajili ya kuweka kumbukumbu, kuandika miradi, na kufuatilia maendeleo kwa njia ya kisasa.
“Sitakuwa kiongozi wa kimazoea. Nitatumia taaluma yangu ya uandishi wa habari kusikiliza na kushirikiana na wananchi kutatua matatizo yao kwa njia ya wazi na ya haki,” amesema Illambona.
Pia, ameahidi kuanza ziara ya kushukuru na kusikiliza wananchi mara tu atakapochaguliwa, na kuteua msaidizi maalum wa kata kwa kusaidia katika uratibu wa shughuli za maendeleo.
“Kata ya Kibimba ina umuhimu wa kimkakati – tuna uwanja wa ndege ambao hata wageni wa kitaifa wanatua hapa. Tukiutumia vizuri, tutaleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi.”
Kwa sasa, watia nia ni watatu, lakini Illambona amesema ana matumaini ya kuungwa mkono na wananchi kutokana na sera zake na maono ya maendeleo ya kweli.
Ametangaza kuwa atachukua fomu rasmi ya kugombea udiwani kupitia CCM tarehe 28 Juni 2025 na kuomba wananchi, pamoja na watu wenye mapenzi mema, kumuunga mkono katika safari yake ya kisiasa.
Mawasiliano:
0756 432 748
0787 089 299
0676 432 748.


