NI SIKU CHACHE ZIMEPITA toka niongelee suala la HAKI za vijana na watu wanaoajiriwa kuchunga Ng’ombe (WACHUNGAJI WA NG’OMBE). Pamoja na kuainisha hitaji la kundi hili kupewa mikataba rasmi lakini pia suala la mateso pamoja na mapito wanayoyapitia ya unyanyasaji nililigusia pia.
Ndugu JUVINARY BARAKA @ MALIATABU mkazi wa Kitongoji cha CHAMBALE, Kijiji cha KUMUGAMBA kata ya NYAKISASA (W) (Mwajiri wa Mchunga Ng’ombe) siku ya Alhamis wiki iliyopita pamoja na mambo mengine yote yaliyotokea siku hiyo alimuadhibu mchungaji wake wa Ng’ombe (anayesadikika kuwa raia wa nchi jirani ya Burundi) kwa :-
- Kumfunga Kamba Miguu na Mikono
- Kumninginiza juu ya mti
- Kumchapa Viboko Vingi sana
Mchungaji wake huyo wa Ng’ombe kosa lake lilisemekana kuwa Ng’ombe amechomwa kisu akiwa machungoni na hivyo kupelekea ng’ombe kufa.
Baada ya Adhabu ile kali Mtoa Adhabu alitafuta namna ya kumfungulia kamba Mwadhibiwa lakini kamba ilikuwa imekaza sana mtini kiasi cha kutofunguka kirahisi na hivyo akaamua kuikata kwa panga (huku mwadhibiwa akiwa bado amening’inia vilevile), kitendo kilichopelekea Mwadhibiwa kudondoka vibaya (akiwa amefungwa vilevile) na kuanza kutoa damu mdomoni na puani. Licha ya kuzidiwa kule, mtoa adhabu inasemekana aliendelea kutoa adhabu hadi baadae mtoto yule (Mchungaji) AKAWA AMEFARIKI.
Mr. JUVINARY BARAKA @MALIATABU alikuwa anatekeleza adhabu hiyo mbele ya Mtoto wake ajulikanaye kama NGEREJA JUVINARY.
Baadae inasemekana Mwenyekiti wa Kitongoji cha CHAMBALE baada ya kuhoji hoji alipewa Tsh 150,000/= ili kusaidia kupoteza ushahidi.
Baada ya Wananchi kupata taarifa hiyo WALIUMIZWA SANA na kitendo hicho kisha wao wenyewe kwakuwa hawakuwa na imani tena na kiongozi wao (M/kiti wa Kitongoji) wakatafuta mgambo kwaajili kumkamata mtuhumiwa ndipo wakafanikiwa kumkamata Jumapili na kumfikishia kituo cha Polisi RULENGE.
Mr. JUVINARY BARAKA @ MALIATABU siku ya Jumatatu alitolewa Dhamana ya Tsh 2,000,000/= (Milioni Mbili tu) baada ya Wadhamini wake kuuza Ng’ombe wake Wawili na Mbuzi kadhaa maana inasemekana wadhamini hao walipewa masaa machache pesa hiyo ya dhamana iwe imepatikana, hadi muda huu Mtuhumiwa yuko Uraiani na Kwa maelezo ya Jamii na Majirani, Mtuhumiwa aliambiwa kulipoti tena kituo cha Polisi Rulenge siku ya Ijumaa wiki hii.
BILA KUINGILIA UTENDAJIKAZI WA JESHI LA POLISI NCHINI kwa uchache sana na kwa ufupi mnoo ninapenda sana na imenipendeza kutumia nafasi hii kumuomba na kumshauri Mkuu wa Jeshi la Polisi (W) Ngara – OCD katika mambo yafuatayo ; –
- KWAMBA, Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCD) RULENGE awajibishwe kinidhamu kwa Uvunjifu wa Taratibu za awali za kiutendaji (Initial Misconducts) alizozionesha kwakuwa Kwa Mujibu wa Kifungu cha 64(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jirani Sura ya 20 Toleo la 2022 ya Sheria za Tanzania, Mdhamana wa Polisi (Police Bail) hutolewa bure. Huyo OCS atapaswa kusema hiyo Milioni Mbili (ikigundulika ni kweli) atakuwa amepokea ya nini kama siyo Rushwa ?
- KWAMBA, wanajamii wanadai kuwa Mtoto wa Mtuhumiwa (PW1) alimshuhudia mtuhumiwa akitekeleza adhabu hiyo inayosadikika kupelekea mauti, kama ni hivyo ninashauri Mtoto huyo atumiwe na Jeshi la Polisi au Jamhuri katika upelelezi kwa kuzingatia Matakwa na Masharti ya Kifungu cha 127 (2), (3) cha Sheria ya Ushahidi Sura ya 6 Toleo la 2022 ya sheria za Tanzania, kinachotoa mazingira mazuri ya kupokelewa kwa ushahidi wa mtoto. Hii itasaidia sana.
- KWAMBA, kwakuwa jamii iliambiwa kuwa mtoto huyo (anayesadikika kuuliwa) hajafa bali alisafirishwa na bodaboda kwenda kwao Burundi, Mtuhumiwa aulizwe vizuri alisafirishwa na boda boda yupi na kwao ni wapi ili ukweli uwe wazi, Kanuni ya 5-W ya Jeshi la Polisi hapa huenda inaweza ikatusaidia kupata majibu mjaarabu kabisa na jamii ikaridhika.
- KWAMBA, Kwa Mujibu wa Kifungu cha 131A(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 Toleo la 2022 ya sheria za Tanzania, hakuna shitaka la jinai litakalopelekwa mahakamani kabla upelelezi haujakamilika. Na katika hili hata ikisemekana upelelezi unaendelea lazima jamii itabaki na dukuduku kwamba kwanini wakati mazingira yote ya tukio yako wazi. Ndugu OCD – Ngara ukiingilia kati katika hili, hata jamii yenye watoto wao ambao ni wachunga Ng’ombe watakushukuru sana na kukuombea.
- KWAMBA, Jamii ya Nyakisasa hadi sasa iko katika Taharuki pamoja na kundi la Wachunga Ng’ombe (W) Ngara. Jeshi la Polisi lisipoonyesha ueledi wake katika hili, kuna uwezekano mkubwa wa jamii ya Nyakisasa kupoteza imani yake kwa jeshi lao hili la Polisi. OCD – NGARA wewe ni mkarimu sana na wanangara tunakutambua kwa sifa hiyo, tunaamini utasaidia katika hili pia.
MWISHO : Kwa Mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 “Kila mtu anayo Haki ya Kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria.”
Tuungane kulinda Haki za Wachungaji wa Ng’ombe nchini, Usalama wao Fahari yetu📍🧎♂️
Mungu Ibariki Ngara!
Mungu ibariki Tanzania!