LINI NGARA ITAPATA USAFIRI WA NDEGE?

By Na Mwandishi Apr 24, 2026

Ndege ya Abiria Yatua kwa Mara ya Kwanza Sumbawanga, Ngara Watoa Wito wa Safari za Ndege


Ndege ya abiria aina ya DASH 8 Q400 inayomilikiwa na Air Tanzania imetua kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga leo Aprili 24, 2026, ikiwa ni sehemu ya hafla ya uzinduzi wa uendeshaji rasmi wa uwanja huo.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ambaye alieleza kuwa uzinduzi huo utarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji katika Mkoa wa Rukwa na kuchochea maendeleo ya uchumi wa eneo hilo.
Amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga ili kufungua fursa zaidi za biashara, uwekezaji na utalii katika maeneo mbalimbali nchini.
Wakati hayo yakijiri, wananchi wa Ngara mkoani Kagera wameiomba Serikali kuanzisha safari za ndege za abiria katika wilaya hiyo ili kurahisisha usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi akiwemo Zawadi Paschal wa Kijiji cha Mukididiri, Joseph Misago wa Kabanga na January Marton wa Kanazi walisema huduma ya usafiri wa anga itawarahisishia wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kwa ujumla kusafiri kwa haraka na kwa ufanisi.
Walisema Ngara ina nafasi ya kipekee kijiografia kutokana na ukaribu wake na mipaka ya nchi za Rwanda na Burundi, huku pia ikihudumia wageni kutoka Democratic Republic of the Congo na Uganda.
Kwa sasa, Uwanja wa Ndege wa Ruganzo unatumiwa zaidi kwa safari maalum zikiwemo zinazohusiana na shughuli za Tembo Nickel Corporation pamoja na safari za viongozi wa Serikali.
Wananchi hao wamependekeza kuanzishwa kwa safari za ndege angalau mara mbili kwa wiki kutoka Ngara kwenda Mwanza au safari ya moja kwa moja hadi Dar es Salaam.
Aidha, wametoa wito kwa viongozi wa wilaya na mkoa, akiwemo Mbunge wa Jimbo la Ngara, Dotto Jasson Bahemu, kulifikisha suala hilo katika ngazi husika za maamuzi Serikalini.
Wamesema iwapo huduma za usafiri wa anga zitaanzishwa, zitachochea ukuaji wa sekta za biashara, utalii na uwekezaji, pamoja na kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri kupitia shughuli za uwanja wa ndege na huduma zake.