NGARA TUTAMBULISHWE KWA NYIMBO ZETU, SIYO ZA BURUNDI NA RWANDA

By Na Mwandishi May 13, 2026


Ndugu mhariri, naomba ufiche jina langu kwa maslahi mapana ya Wana Ngara.
Ngara ni wilaya iliyopo kaskazini-magharibi mwa Tanzania katika Mkoa wa Kagera, ikikaliwa zaidi na makabila ya Wahangaza na Washubi wenye utamaduni wao wa kipekee unaostahili kuhifadhiwa, kuenziwa na kutambulishwa kizazi hadi kizazi.
Naandika ujumbe huu kwa masikitiko, lakini pia kwa nia njema ya kuamsha ari na vuguvugu la kuuenzi utamaduni wetu wa asili kupitia muziki wetu wenyewe.
Imekuwa jambo la kawaida katika shughuli mbalimbali za kijamii kama harusi, sherehe na matukio ya kitamaduni yanayowakutanisha Wana Ngara, kusikia ma-DJ na ma-MC wakipiga nyimbo kutoka Burundi na Rwanda badala ya nyimbo zinazotambulisha tamaduni za Wahangaza na Washubi.
Hakuna ubaya kuthamini muziki wa jirani zetu, lakini inapofikia hatua ya shughuli zinazotutambulisha sisi kujaa nyimbo za wengine huku muziki wetu ukisahaulika, hapo tunakuwa tunadhoofisha utambulisho wetu wa kitamaduni.
Ikiwa baadhi ya ma-DJ hawana hazina ya kutosha ya nyimbo za asili za Ngara, basi ni bora hata kuwaalika vikundi vya utamaduni au watu wenye uwezo wa kuimba moja kwa moja (live) ili kuonesha utamaduni wetu halisi.
Nitoe wito kwa Wana Ngara wote — wasanii, wazee wa mila, viongozi wa jamii na vijana — tuungane kuandaa matamasha ya utamaduni, kurekodi nyimbo zetu za asili na kuhakikisha zinapatikana kwa urahisi katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Ngara ina utamaduni mkubwa na wa kujivunia. Tusikubali upotee kwa kuiga zaidi tamaduni za wengine wakati sisi pia tunayo ya kwetu yenye thamani kubwa.
Asanteni.
Murantunga