
Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Ngara wameungana na mashabiki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kushangilia matokeo ya sare ya mabao 1-1 dhidi ya Ureno katika Michuano ya Kombe la Dunia 2026.
Wakizungumza na Ngara TV, baadhi ya mashabiki akiwemo Liberatus Richard, Gilman Jovitho na Siwema Mathayo, walisema matokeo hayo ni makubwa kwa DRC kutokana na nguvu na ubora wa timu ya taifa ya Ureno.
“Wengi walitarajia DRC kufungwa, lakini wameonyesha uwezo mkubwa na kupambana hadi mwisho,” alisema mmoja wa mashabiki hao.
Katika mchezo huo wa Kundi K uliopigwa katika dimba la Houston, Texas nchini Marekani, Ureno walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia João Neves dakika ya 6 kabla ya DRC kusawazisha kupitia mshambuliaji Yoane Wissa katika dakika ya 45+5.
Bao la Wissa limeandika historia kwa kuwa bao la kwanza kufungwa na mchezaji wa DRC katika fainali za Kombe la Dunia. Mafanikio hayo yamehitimisha kusubiri kwa zaidi ya nusu karne tangu taifa hilo liliposhiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo mwaka 1974 likiitwa Zaire na kuondoka bila kufunga bao lolote.
Matokeo hayo yamepokelewa kwa furaha kubwa na mashabiki wa DRC pamoja na wadau wa soka barani Afrika, ambao wanaona kuwa ni hatua muhimu kwa taifa hilo katika michuano ya Kombe la Dunia 2026.
Matokeo KamiliFT: Portugal 1-1 DRC
⚽ João Neves 6′
⚽ Yoane Wissa 45+5′
