
Ndugu yangu mwana Ngara,
Leo naomba nikushirikishe tafakari kuhusu ndege aina ya Pelikani, ambaye katika mapokeo ya kale ya Kikristo amekuwa ishara ya upendo wa kujitoa mhanga.
Hadithi hiyo inaeleza kwamba wakati wa njaa kali, mama pelikani alidaiwa kujijeruhi kifua chake ili kuwalisha watoto wake kwa damu yake badala ya kuwaacha wafe kwa njaa. Ingawa simulizi hili ni la mfano wa kiimani, limekuwa na maana kubwa katika Ukristo kwa karne nyingi.
Kwa sababu hiyo, Pelikani amekuwa alama inayomwakilisha Yesu Kristo, aliyemwaga Damu yake kwa ajili ya wokovu wa wanadamu.
Picha ya ndege huyu anayewalisha watoto wake imekuwa ikitumiwa kufundisha kuhusu upendo, sadaka na kujitoa kwa ajili ya wengine.
Neno la Mungu linasema:
“Upendo ulio mkuu zaidi mtu alio nao ni huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yohana 15:13)
Mafundisho haya yanatukumbusha kuwa upendo wa kweli unaambatana na kujitoa, huduma na kujali wengine hata pale inapohitaji sadaka binafsi.
Ndugu wananchi wa Wilaya ya Ngara, katika kipindi hiki tunachojenga maisha na maendeleo ya jamii yetu, tunaalikwa kuishi mafundisho haya kwa vitendo.
Tuwapende jirani zetu, tusaidiane wakati wa shida, tushirikiane katika shughuli za maendeleo, na tujenge mshikamano unaotuwezesha kusonga mbele kama jamii moja.
Maendeleo ya Ngara hayatajengwa na mtu mmoja, bali na moyo wa umoja, ushirikiano na kujitolea kwa manufaa ya wote. Kila mmoja wetu ana mchango wa kutoa, iwe ni mawazo, nguvu kazi, maarifa au rasilimali alizonazo.
Tukitanguliza upendo na mshikamano, tutaimarisha familia zetu, vijiji vyetu na Wilaya yetu kwa ujumla.
Naamini kuwa Ngara yenye watu wanaopendana, kusaidiana na kushirikiana ni Ngara yenye matumaini makubwa ya maendeleo endelevu kwa kizazi cha leo na kijacho.
Mungu aibariki Ngara. Mungu awabariki wananchi wote wa Wilaya ya Ngara.
Wenu,
Juventus Juvenary Illambona
