
Wananchi wa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera wametakiwa kuongeza umakini na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola unaodaiwa kuripotiwa katika baadhi ya maeneo ya nchi jirani za Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Kanali Mathias Julius Kahabi, wakati akizungumza na wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Chama Kipya cha Ushirika wa Msingi cha Rulenge AMCOS Limited.
Kanali Kahabi amesema kuwa kutokana na jiografia ya Wilaya ya Ngara kuwa karibu na mipaka ya nchi jirani, wananchi wanapaswa kuwa makini zaidi kwa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima pamoja na kugusana mara kwa mara wakati wa salamu na shughuli nyingine za kijamii.
“Ni muhimu wananchi kuchukua tahadhari mapema ili kujilinda na kuwalinda wengine dhidi ya hatari ya maambukizi,” amesema Kanali Kahabi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Ramadhan Yahya Kido, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko yanahitaji ushirikiano wa kila mwananchi.
Kanali Kido amesema Wilaya ya Ngara ipo katika eneo la kimkakati linalopakana na Uganda, Burundi na Rwanda huku ikiwa karibu pia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hali inayoongeza umuhimu wa wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.

Aidha, amewahimiza wananchi kuendelea kuzingatia usafi binafsi, kutoa taarifa mapema kwa mamlaka za afya wanapoona dalili zinazotia shaka, na kufuata elimu inayotolewa na wataalamu ili kuzuia hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo.
