DOTTO BAHEMU ASHIRIKI KIKAO CHA MAENDELEO YA MICHEZO WILAYANI NGARA

By Na Mwandishi Jul 21, 2026

Na, Juventus Juvenary-Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ngara.

Mbunge wa Jimbo la Ngara, Mheshimiwa Dotto Jasson Bahemu, ameshiriki kikao cha wadau wa michezo kilicholenga kujadili maendeleo ya sekta ya michezo wilayani Ngara na kuweka mikakati ya kuikuza zaidi.

Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Wilaya ya Ngara na kuhudhuriwa na Afisa Utamaduni na Michezo wa Wilaya, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ngara (NDFA) ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kabanga, Bw. Hafidh Abdallah, viongozi wa vilabu vya soka pamoja na wadau mbalimbali wa michezo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Dotto Jasson Bahemu ameahidi kushirikiana kwa karibu na viongozi na wadau wote wa michezo ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua na kutoa fursa kwa vijana wa wilaya hiyo.

Mbunge Bahemu pia ametangaza dhamira yake ya kuanzisha Mashindano ya Kombe la Mbunge wa Jimbo la Ngara, yatakayofanyika kuanzia kwenye ngazi ya Kata hadi wilaya, yakilenga kuibua vipaji, kuhamasisha ushiriki wa vijana katika michezo na kuimarisha mshikamano wa jamii.

Aidha, amesisitiza kuendelea kuunga mkono juhudi za Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ngara (NDFA) na wadau wengine ili kuhakikisha Wilaya ya Ngara inafanya vizuri katika Ligi ya Daraja la Nne, hatua ambayo itaongeza ushindani na kukuza kiwango cha soka wilayani humo.