C.d.e Eliud Amon Ruzige awiwa kuwatumikia wanangara, atangaza nia kugombea Ubunge jimbo la Ngara

By Titho Philemon May 8, 2025

Akiongea na Ngaratv.com C.d.e Eliud Amon Ruzige amesema kuwa Jimbo la Ngara linahitaji mapinduzi makubwa sana ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ili kuweza kujipatia maendeleo, na hivyo ni wakati sahihi wa wazalendo wa Ngara kuungana na kuona ni kwa namna gani wataweza kuweka nia ya pamoja ya kuudhihirisha utofauti kupitia uchaguzi mkuu wa Octoba mwaka huu kwa kujipatia kiongozi bora atakayeweza kuondoa mkwamo wa kiuchumi na kijamii ambao umewashinda viongozi waliotangulia.

Katika hatua nyingine, C.d.e Eliud Amon Ruzige alivyohojiwa na Ngaratv.com kuhusu nia yake ya kugombea ubunge wa Jimbo la Ngara Mwaka huu amesema,

Nanukuu ;-

Ndugu Mwandishi, ni kweli nia ninayo na kwakuwa ninapenda kuiona Ngara ikipiga hatua kutoka hapa ilipo, nimeona vema nami nishiriki tukio hili la kizalendo na la kiraia la kugombea Ubunge na panapo majaliwa niwe miongoni mwa wazalendo wenzangu watakaoshiriki katika kinyang’anyiro hiki lengo ikiwa ni kuijenga upya Ngara yetu. Mimi ni kada mwaminifu wa Chama cha Mapinduzi, ninakiu sana ya kuona Ngara inafika mbali, ofcourse nimekuwa nikisaidia kujenga chama na serikali hasahasa jimbo langu la Ngara, kwahiyo chama kitakapoanza taratibu zake za kutoa fomu nami nitakuwa miongoni mwa watakaoshiriki”

Kwa wasiomfahamu, kwa ufupi C.d.e Eliud Amoni Ruzige ni mzaliwa wa kijiji cha Chivu, kata ya Ntobeye, wilaya ya Ngara, mkoani Kagera (Tanzania). Amebahatika kupata elimu yake ya Msingi katika Shule ya Msingi Chivu (Ngara DC), Elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Kahororo (BUKOBA DC), Elimu ya sekondari ya Upili (High School) katika Shule ya Sekondari USA RIVER (Arusha). Katika kuendelea na Elimu ya Juu C.d.e Eliud Amon Ruzige alisoma na kutunukiwa Shahada ya Kwanza ya Fedha na Uchumi (Bachelor of Finance and Accounting with Economics) katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania (SAUT) – Mwanza.

Kuhusu siasa, C.d.e Eliud Amon Ruzige amejiunga na Chama cha Mapinduzi mwaka 2011 akiwa mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania (SAUT), Mwaka 2012 akachaguliwa kuwa Katibu wa Tawi wa CCM wa Tawi la SAUT, pia alikuwa ni Mjumbe wa Kamati ya utekelezaji wa UVCCM wilaya ya Nyamagana hadi alipomaliza chuo kikuu.

Ndani ya Siasa za Ngara, C.d.e Eliud Amon Ruzige Mwaka 2017 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Mkutano Mkuu wa kata akitokea kata ya Ntobeye hadi Mwaka 2022. Mwaka 2022 kupitia uchaguzi wa ndani ya chama kwa mwaka huo alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya kutokea kata ya Ntobeye. Hadi sasa C.d.e Eliud Amon Ruzige ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Fedha ambayo iko chini ya Jumuiya ya Wazazi wa CCM wilaya ya Ngara ambapo kupitia kamati hiyo wameweza kufanikiwa kufanya mambo mengi ya ujenzi na uimarishaji wa chama Ngara.

Kijamii, C.d.e Eliud Amon Ruzige chini ya Taasisi yake ya Elimu ijulikanayo kama Moonshine Training Institute (MTI) chuo kinachopatikana wilayani Ngara, amefanikiwa kujitolea kusomesha bure baadhi ya wanafunzi wanaotokea katika mazingira magumu, lakini pia uwepo wa taasisi yake ya chuo ndani ya eneo la Ngara licha ya kuongeza idadi ya watu Ngara, imepanua wigo mkubwa na kuchochea ukuaji wa kiuchumi kwa maana ya kuongeza pato la wanangara. Lakini kupitia Taasisi yake ndani ya Ngara amejaribu kulipa fadhira kwa jamii (CSR) kupitia kufanya usafi kwenye masoko, kuchangia damu hospitalini pamoja na mambo mengine mengi.

Aidha, C.d.e Ruzige ameiambia Ngaratv.com kuwa nia yake ni ya dhati na wala hajaribu bali amedhamiria. Kama ambavyo amekuwa akiguswa na wanangara, anaamini kutia kwake nia kunaweza kufungua njia ya yeye kuhusika kikamilifu katika kuhakikisha adhima na maendeleo ya kweli Ngara yanapatikana.

Endelea kufuatilia Taarifa zetu Ngaratv.com kwa habari zaidi..!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *