


Na Juventus Juvenary – Dodoma.
Treni ya kisasa ya umeme maarufu kama “Mchongoko” imeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa Watanzania kutokana na kasi, ubora na muonekano wake wa kipekee katika reli ya kisasa ya SGR nchini Tanzania.
Jina la “Mchongoko” limetokana na muundo wa mbele wa treni hiyo unaofanana na mdomo wa mchongoko.
Treni hiyo ni aina ya Electric Multiple Unit (EMU) inayotumia umeme badala ya dizeli, hatua inayotajwa kuwa sehemu ya mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri wa reli nchini.
Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania ilianzisha mradi wa reli ya kisasa ya SGR kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri wa abiria na mizigo pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Mwaka 2024, seti ya kwanza ya treni hizo iliwasili kupitia Bandari ya Dar es Salaam kabla ya kuanza rasmi kutoa huduma za usafiri kati ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.
Treni hiyo yenye uwezo wa kwenda hadi kilomita 160 kwa saa, pia ina uwezo wa kubeba zaidi ya abiria 500 kwa safari moja, jambo lililorahisisha usafiri wa wananchi na kupunguza muda wa safari kati ya miji mikubwa.
Kwa sasa, “Mchongoko” imekuwa moja ya alama za maendeleo ya teknolojia ya usafiri nchini huku ikivutia mataifa mbalimbali barani Afrika kujifunza mfumo wa reli ya kisasa wa Tanzania.
