WAKULIMA WASHANGILIA

Na, Juventus Juvenary
Historia mpya imeandikwa Wilayani Ngara baada ya kuzinduliwa kwa Chama kipya cha msingi cha Rulenge AMCOS Limited, hatua inayotajwa kuwa chachu ya maendeleo kwa wakulima na wananchi kwa ujumla.
Uzinduzi wa Rulenge AMCOS Limited umefanyika Mei 22, 2025 ambapo mgeni rasmi alitarajiwa kuwa Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo, lakini akawakilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Ramadhan Yahya Kido.
Akisoma taarifa ya AMCOS hiyo, Mwenyekiti wa Bodi, Injinia Deusdedith Kakoko amesema kuanzishwa kwa chama hicho ni ukombozi mkubwa kwa wananchi hususan wakulima wa mazao ya mahindi, maharage, alizeti, parachichi na kahawa.
Amesema Rulenge AMCOS Limited inalenga kuwaunganisha wakulima, kuongeza tija ya uzalishaji, kuboresha masoko ya mazao pamoja na kuinua uchumi wa wananchi kupitia mfumo wa ushirika wenye manufaa kwa wanachama wake.
Wananchi na viongozi mbalimbali waliohudhuria uzinduzi huo wameeleza matumaini yao kuwa AMCOS hiyo itasaidia kuondoa changamoto za masoko, unyonyaji wa bei na kuongeza kipato kwa wakulima wa Wilaya ya Ngara.




