
Na, Juventus Juvenary Illambona-Ngara.
Siku moja nikiwa nimepumzika nyumbani, wazo la ghafla lilinijia kichwani la kupitia makabrasha na nyaraka zangu mbalimbali za kumbukumbu.
Nilipoanza kupanga vitabu vyangu, nikakutana na kijitabu kilichoandikwa “Changamoto za Maendeleo ya Wilaya ya Ngara.”
Kijitabu hicho kinabeba kumbukumbu za semina iliyofanyika tarehe 31 Desemba 2011 katika Ukumbi wa Maria, Rulenge, wilayani Ngara.
Napenda kutoa shukrani za dhati kwa Jukwaa la Uhamasishaji wa Maendeleo Ngara (JUMAN) kwa kuandaa na kuhifadhi kumbukumbu hizi muhimu. Bila juhudi hizo, mengi yaliyofanywa na viongozi wetu yangeweza kusahaulika.
Lengo la andiko hili ni kumpongeza na kumshukuru aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ngara wakati huo, Mheshimiwa Deogratias Ntukamazina.
Kupitia semina hiyo, iliyoandaliwa chini ya uratibu wa Ndugu Pius Ngeze, Mheshimiwa Ntukamazina alitoa hotuba ya ufunguzi iliyojikita katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya Wilaya ya Ngara.
Kama ambavyo amekuwa akisisitiza tangu alipochaguliwa kuwa mbunge, aliweka wazi dhamira yake ya kupambana na maadui watatu wa maendeleo: ujinga, maradhi na umasikini.
Wananchi wa Ngara watakumbuka kuwa miongoni mwa hatua zake za mwanzo akiwa mbunge ilikuwa ni kuwawezesha wajasiriamali kwa kuleta wataalamu wa kutoa mafunzo ya ujasiriamali pamoja na elimu ya kuanzisha Benki za Kijamii Vijijini (VICOBA).
Lengo lilikuwa kukuza kipato cha wananchi kupitia vikundi vya uzalishaji na uwekezaji.
Mheshimiwa Ntukamazina alitambua kuwa pato la wananchi wa Ngara lilikuwa chini ukilinganisha na baadhi ya wilaya nyingine za Mkoa wa Kagera, licha ya wilaya hiyo kuwa na ardhi yenye rutuba na mvua za kutosha. Kutokana na hali hiyo, aliwahimiza wafanyabiashara kushiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo, akisisitiza kuwa kilimo ndicho uti wa mgongo wa uchumi wa wilaya.
Leo hii, wafanyabiashara wengi wa Ngara wanajihusisha na kilimo cha kahawa, parachichi, migomba, mahindi na maharage pamoja na shughuli za ufugaji.
Aidha, aliwahamasisha wananchi kutumia mabonde yaliyopo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao.
Katika kuunga mkono azma hiyo, alimwalika aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Eng. Christopher Chiza, ambaye pia alikuwa Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kutembelea mabonde ya Ngara ili kutathmini uwezekano wa kuyaendeleza kwa kilimo cha umwagiliaji.
Miradi mingine iliyopata kuzungumzwa katika kipindi hicho ni pamoja na mradi wa Mgodi wa Nikeli, ambapo wananchi walihimizwa kujiandaa kupata ajira na kuzalisha bidhaa zitakazohitajika mgodini.
Pia, kulikuwa na matarajio ya ujenzi wa reli itakayounganisha Tanzania, Rwanda na Burundi, ambapo ilielezwa kuwa hatua za upembuzi yakinifu na usanifu zilikuwa zimefanyika.
Mheshimiwa Ntukamazina aliwasihi wananchi kufuatilia fursa za ajira zitakazotokana na miradi hiyo na kuongeza uzalishaji wa kiuchumi ili kuitumia reli hiyo kama chachu ya maendeleo ya Ngara na taifa kwa ujumla.
Wananchi wa vijiji vya Buhororo na Munjebwe pia watanukuu mchango wake katika utekelezaji wa4 mpango wa MKURABITA, ambapo baadhi yao walipata hati za kimila za umiliki wa ardhi.
Hatua hiyo ilitarajiwa kurahisisha upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za kifedha, ikiwemo benki, kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Yapo mengi aliyofanya. Mengine tofauti na niliyokutajia ni pamoja na kusaidia kupanua huduma za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) ili kuwafikia wananchi wengi zaidi ambapo alimuomba Mkurugenzi Mkuu wa TASAF kuhakikisha kuwa huduma hiyo inasambazwa katika vijiji vyote vya Wilaya ya Ngara, jambo ambalo lilitekelezwa.
Aidha, aliomba kuteuliwa kwa afisa mmoja katika Halmashauri atakayesimamia uratibu wa wataalamu kutoka TASAF Makao Makuu.
Katika sekta ya ardhi, Mheshimiwa Ntukamazina aliwasilisha ombi kwa Waziri wa Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka, la kuanzishwa kwa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Ngara ili kupunguza adha kwa wananchi waliokuwa wakisafiri hadi Chato kufuatilia mashauri yao ya ardhi, na Ombi hilo lilikubaliwa na hatua zikachukuliwa kulitekeleza.
Kwa kutambua umuhimu wa elimu na maarifa katika maendeleo ya jamii, alimuomba Mkurugenzi Mkuu wa Maktaba ya Taifa kuanzisha maktaba mbili wilayani Ngara.
Maktaba hizo, moja ikiwa ya Wilaya na nyingine ya Tarafa ya Rulenge, zilianzishwa mwaka 2013 kwa lengo la kuwahudumia wanafunzi pamoja na vijana na watu wazima wanaotaka kujiendeleza kielimu na kuongeza maarifa yao.
Katika kuboresha elimu, aliwasilisha maombi kwa Wizara ya Elimu ili kupatikane walimu wa kujitolea kutoka Marekani kufundisha masomo ya Sayansi na Kiingereza. Walimu wanne walipatikana, ambapo wawili walifundisha katika Shule za Sekondari za Murgwanza na Ngara Mjini, huku wawili wengine wakipelekwa katika shule za Muyenzi na Nyakisasa.
Walihudumu kwa kipindi cha miaka miwili.
Kuhusu Mradi wa Kabanga Nickel, Mheshimiwa Ntukamazina aliendelea kuibana Serikali kutokana na kusuasua kwa utekelezaji wa mradi huo.
Mwaka 2014, Serikali ilimtuma nchini Canada kufanya mazungumzo na viongozi wa Barrick Gold ili kupata ufafanuzi kuhusu kuchelewa kwa mradi huo.
Baada ya mazungumzo hayo, alibaini kuwa kampuni hiyo ilikuwa na mwelekeo mkubwa zaidi katika uchimbaji wa dhahabu kuliko nickel.
Aliporejea nchini, alipendekeza Serikali kutafuta mwekezaji mwenye uzoefu na nia ya kuendeleza uchimbaji wa nickel, na Serikali ilikubaliana na pendekezo hilo.
Katika sekta ya kilimo, alimwomba Waziri wa Kilimo wa wakati huo, Mheshimiwa Christopher Chiza, kuiingiza Wilaya ya Ngara katika orodha ya wilaya zilizonufaika na mpango wa pembejeo za kilimo.
Ombi hilo lilipokelewa na kutekelezwa.
Kupitia Mfuko wa Jimbo, Mheshimiwa Ntukamazina aliongoza ujenzi wa visima vinne vya kuvuna maji ya mvua katika shule za sekondari zilizokuwa zikikabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji.
Shule hizo ni Sekondari za Muruvyagira, Kanazi, Ndomba na Nyakisasa.
Aidha, alifanikiwa kushirikiana na Serikali pamoja na Ubalozi wa Uholanzi (Netherlands) katika upatikanaji wa jenereta mbili kubwa za kuongeza uwezo wa usambazaji wa umeme wa TANESCO wilayani Ngara.
Katika juhudi za kupeleka umeme vijijini, aliishawishi Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuanza utekelezaji wa miradi ya umeme katika maeneo ya Mugoma, Rusumo, Benaco na Rulenge kabla ya kumalizika kwa kipindi chake cha ubunge mwaka 2015.
Maombi hayo yalitekelezwa. Vilevile, aliiomba REA kujenga kituo kidogo cha kupozea na kusambaza umeme (substation) katika eneo la Djuruligwa ili kuongeza uwezo wa usambazaji wa umeme katika maeneo ya Rulenge na Kabanga.
Hatimaye, transfoma kubwa ililetwa kutoka TANESCO Arusha na kufungwa katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Ntukamazina, amesema mwaka 2013 alipata fursa ya kuwasilisha kwa Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, baadhi ya changamoto na mahitaji ya maendeleo ya Wilaya ya Ngara wakati wa ziara yake wilayani humo.
Akizungumza kuhusu baadhi ya mafanikio na changamoto alizokutana nazo akiwa mbunge, Ntukamazina alisema Rais Kikwete alipowasili Ngara akiwa ameambatana na mawaziri saba, alimweleza umuhimu wa kuipandisha hadhi Rulenge kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo, jambo ambalo baadaye lilikubaliwa na Serikali.
Aidha, alisema katika kikao kilichofanyika Ngara Mjini, alimweleza Rais kuhusu changamoto ya upatikanaji wa maji iliyokuwa ikikabili wananchi kutokana na uchakavu wa mitambo ya maji ya Ngara Heights.
Kwa mujibu wa Ntukamazina, Rais Kikwete alimwagiza aliyekuwa Waziri wa Maji wakati huo, Profesa Jumanne Maghembe, kufuatilia suala hilo. Baadaye, wizara ilitoa shilingi milioni 200 kama fedha za awali kwa ajili ya ukarabati wa mitambo hiyo.
Hata hivyo, Ntukamazina alidai kuwa sehemu ya fedha hizo ilitumiwa kinyume na taratibu na kwamba alihakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa. Alisema kuchelewa kwa mashauri ya aina hiyo kuamuliwa kunadhoofisha juhudi za kupambana na ubadhirifu wa fedha za umma.
“Ni vigumu kupata maendeleo ya kweli ikiwa wizi wa rasilimali za umma na matumizi mabaya ya fedha za wananchi hayatachukuliwa hatua kwa wakati,” alisema.
Ntukamazina alisisitiza kuwa uwajibikaji wa viongozi na watendaji wa umma ni nguzo muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inawanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.
Hakika, Mheshimiwa Deogratius Ntukamazina ameacha alama katika historia ya maendeleo ya Wilaya ya Ngara.
Kwa mchango wake katika kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kutafuta fursa za maendeleo, anastahili kukumbukwa na kuthaminiwa.
Ngara inakushukuru na inakutakia afya njema

