Mara baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kupuliza kipenga kwa kutangaza kuanza kwa michakato ya chaguzi na teuzi ndani ya chama kuelekea uchaguzi Mkuu 2025, wananchi, wanachama na watia nia wa nafasi za Ubunge na Udiwani nchini wamekuwa na fikra mseto.
Wapo wanachama wa CCM na wananchi wanaowaza kuhusu upatikanaji wa kiongozi bora, lakini vilevile wapo watiania bila kujali ukubalifu wao kijamii wanaozidi kujiimarisha kiuchumi kwaajili ya kukabiliana na mchakato huo.
Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Ngara Ndugu NDAISABA GEORGE RUHORO siku ya jana (April 10, 2025) mara baada ya kutolewa kwa Tangazo rasmi la chama kuhusu kuanza kwa michakato ya uchaguzi ndani ya chama amechapisha waraka huo katika ukrasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa Facebook akiambatanisha na nia ya kugombea tena awamu nyingine ya uwakilishi kwa Mwaka 2025/2030, nanukuu ujumbe wake:-
“NINACHUKUA FOMU TENA KUENDELEZA KAZI NZURI NILIYO ANZA NAYO 2020”
Chapisho la kutangaza nia la Mheshimiwa huyu limepata uungwaji mkono kwa maoni Rukuki (Comments) kuliko machapisho yake yote ambayo ameyachapisha kwenye mtandao huo toka kuanza kwa mwaka huu. Ni mapema sana kuamini kuwa wingi wa maoni hayo yaliyodhihirisha hisia za upendo dhidi ya Mbunge huyu ni ya kweli au siyo ya kweli hadi pale zoezi la kura za maoni litakapotamatika ndani ya chama na kutupa dalili halisi za uhalali wa siasa zake, mapokeo na mvuto alionao mbunge huyu kwa wananchi wa jimbo la Ngara.
Kwa Msingi wa Tafakuri yangu Tunduizi kama mwanachama wa CCM na Mwananchi mzalendo wa Jimbo la Ngara, kuna mambo makuu Manne (4) ambayo yamenitafakarisha kisawasawa;-
- Kwanini Asilimia kubwa ya Wanangara waishio nje ya Ngara hawafurahishwi na uongozi wake ? Je pengine ni (1)Kwasababu hawako jimboni kupima na kuona kilichofanywa na Mbunge huyu? (2) Kwasababu utendaji kazi wake haujathibitika kiasi cha kuitangaza Ngara kwenye uga wa kitaifa na kimataifa (3) Hajaeneza Matunda thabiti ya asili na uasili wa Wanangara katika misingi ya kuwajengea heshima kitaifa kupitia uwakilishi wake ? (4) Au pengine wanaona na wanaamini hakuna alichokifanya zaidi ya maigizo kama wanavyosema. Hakika nimetafakari sana!
- Kwanini Wazee na Manguli wa siasa za Ngara na Tanzania hawavutiwi na siasa zake ? Mheshimiwa Mbunge amekuwa na ukubalifu mkubwa sana kwa Wazee wa Vijijini tena wengi sana wakiwa wale ambao uelewa wao ni wa chini sana (Cheap and Illiterate Group of Elders – CIGE) huku watangulizi wake wakimpiga vita. HII INATOKANA NA NINI ? Je ni kweli amekosana nao na kujenga nao mazingira magumu kiasi cha wao kutokukubali kumuunga mkono kwa lolote ? BADO NIKAZIDI KUTAFAKARI!
- Tafakuri yangu Tunduizi imepima na kukubali ukweli kwamba zaidi ya 70% ya wajumbe na Wapiga kura ( Kwa mjumuisho wa Rika zote na Jinsia zote) ndani ya Jimbo la Ngara wanamkubali na wana imani naye katika maeneo aliyowahi kupita, lakini kuna baadhi ya maeneo machache aliwahi kupita akatafsiriwa katika dhana ya ubaguzi wa rangi, ulemavu na kutoheshimu jitihada za watangulizi wake huku akiwa amejingea msimamo kupitia tamko lake la kwamba kabla yake Ngara ilikuwa imetengwa kama jangwa. Bado ninatafakari, Je hayo maeneo aliyoyatia majeraha hayatomuathiri na kusambaza sumu za kumdhoofisha kisiasa ? Je hata akisema aanze kujisafisha na kuwaomba msamaha aliowakwaza, kwasasa itasaidia chochote? Je muda unatosha kwa yeye kujisafisha ? BADO NATAFAKARI!
- BADO NATAFAKARI, Je ikitokea asiombe radhi kwa wale aliowajeruhi kwa kauli zake tata, na kuwaomba wanajamii kumsamehe, katika hilo haoni kama kelele za unyanyapaa zinaweza kushinikiza msisimko na maamuzi ya tofauti kwenye kamati za maamuzi na uteuzi na hivyo kumkosesha sifa stahiki za kuteuliwa ndani ya chama katika nafasi yake ya ubunge kwa awamu ya pili ya 2025/2030?
Kupitia Tafakuri yangu Tunduizi NIMETAMBUA na KUHESHIMU uwepo wa vyama vingine vya siasa ndani ya Jimbo la Ngara, na kiu ya chama changu CCM ya kutokupoteza utawala.

Kwahiyo, ni muda wa chama cha Mapinduzi kutafakari hali hii ya kisiasa kwa Jimbo la Ngara, na kuhakikisha jitihada za dharura na za maksudi zinafanyika ili kuondoa mikwamo sugu iliyojificha ndani ya vita ya siasa za ubunge ndani ya CCM Ngara na ndani ya Jimbo la Ngara.
BADO NATAFAKARI, bila NDAISABA Ngara itaongozwa na nani kwa 2025/2030 ? Ila napata majibu kuwa, kila NATI ina SPANA yake. Tukikosa SPANA maalumu tutatumia hata ile ya MATUNDU MENGI, kikubwa Jimbo litawalike!
Aidha, KWA KUMALIZIA TAFAKURI yangu, ninampongeza sana Mheshimiwa NDAISABA GEORGE RUHORO Mbunge wa Jimbo la Ngara kwa uthubutu na uamuzi wake wa kutangaza nia kugombea nafasi ya ubunge kwa mara nyingine. Huo nao ni ushujaa!
Ninaomba niishie hapa, na hiki kilichoandikwa kichukuliwa kama Mawazo huru ya mwandishi na NI FIKRA ZANGU TU, na hivyo ninasimama kukosolewa na kuelekezwa pale itakapobidi!
🔰💚💚💚🇹🇿🧎♂️🙏