Taifa la Tanzania na watanzania wote tukiwa tumebakiza miezi michache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kuna haja kubwa ya viongozi wa dini nchini kuendelea kusisitiza utawala wa sheria nchini ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya uchaguzi kwa waumini wao.
Taifa letu la Tanzania kwa mwaka 2019, 2020, na 2024 limeshuhudia kufanyika kwa chaguzi mbalimbali nchini ambazo siyo huru, zisizo za haki na zisizohusisha utashi kamili wa wapiga kura kama lilivyotakwa la kisheria na la kidemokrasia.
Tabia hii ya kuwa na Demokrasia bubu imekuwa ikiwakwaza watanzania wengi huku nchi ikigubikwa na matukio ya hovyo yanayohusisha kutekwa kwa wanasiasa wa upinzani na baadhi ya wanaharakati wasioiunga mkono serikali na chama tawala (CCM).
Viongozi wa dini hapa nchini ndio watu pekee walioshikiria taasisi za kiimani nchini ambao wanauwezo wa kuwahubiria amani na Utawala wa sheria waumini wao na viongozi wa nchi na wakaelewa kwa kigezo cha hofu ya Mungu. Kwahiyo, wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha wanafundisha maadili ya kimungu kwa baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi na Taasisi zao ili kuepuka uhaini wa hisia za Watanzania unaofanywa na watawala wetu nchini wakiwemo viongozi wakuu ndani ya chama tawala na serikali.
Imani ya watanzania imebakia Misikitini na siyo ndani ya serikali yao kwa sasa. Imani ya Watanzania imesalia makanisani na siyo serikalini. Kwahiyo, kuna kila sababu ya wakuu wa taasisi hizo za kiimani na kidini kuhakikisha wanaendelea kusisitiza utawala wa sheria katika taifa letu bila wasiwasi wala hofu binafsi ili kuhakikishia kuwa ustawi mpya na uhuru wa kisiasa hapa nchini unapatikana na hatimaye watanzania waweze kuwapata wawakilishi na viongozi watokanao na utashi wao.
Tanzania ni yetu sote, Usalama wetu uko mikononi mwetu.
Bila uchaguzi halali na haki hakuna taifa la watu bali litakuwa taifa la watawala. Viongozi wa dini lisaidieni taifa letu katika suala nyeti hili la uchaguzi ambalo litakuwa na matokeo chanya au hasi yenye athari kwa watanzania wote kwa miaka ipatayo mitano.
Asanteni sana🙏