MZEE EDWARD MABARANKURU WA BUHORORO AMEFARIKI.

By Na Mwandishi May 9, 2026

Jamii ya Wana Buhororo, Kijiji cha Buhororo Kata ya Kibimba Wilaya ya Ngara kwa mara nyingine inapitia kipindi cha huzuni kufuatia kifo cha Mzee Edward Mabarankuru aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 82.

Kwa masikitiko makubwa, www.ngaratv.com⁠ inaungana na familia, ndugu, jamaa na wananchi wa Buhororo baada ya kupokea taarifa za kifo hicho kilichotokea jana Ijumaa usiku majira ya saa 9 akiwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamiaga.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini amesema kuwa kifo hicho ni pigo kubwa kwa jamii kutokana na mchango mkubwa aliokuwa ameutoa katika malezi, ushauri na kuimarisha mshikamano wa kijamii.

“Hakika huu ni msiba mkubwa kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki waliobahatika kuishi naye na kujifunza mengi kupitia busara, malezi na nasaha zake zilizogusa maisha ya wengi,” amesema mwananchi huyo.

Wananchi mbalimbali wameeleza kuwa Mzee Edward Mabarankuru atakumbukwa kwa upendo, hekima na moyo wake wa kusaidia jamii, huku wakisisitiza kuwa maneno na ushauri wake vitaendelea kuishi mioyoni mwa watu wengi aliowagusa katika maisha yake.

“Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana lihimidiwe.”.

Pumzika kwa amani Mzee wetu Edward Mabarankuru. Mungu awape faraja na uvumilivu wote walioguswa na msiba huu