Vijana wa Kagera Tuungane kuwakataa wanasiasa wababaishaji uchaguzi Mkuu 2025

By Titho Philemon Feb 24, 2025

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa 2025 hapa nchini, vijana wa Mkoa wa Kagera tunapaswa kushikamana kwa umoja wetu kukemea na kuwakataa viongozi wote ambao kwa miaka yao yote ya kiutawala hawakuwahi kukamilisha furaha ya wanajamii na wapiga kura wanaowaongoza wakati walikuwa katika nafasi, uwezo, nia na sababu ya kufanya hivyo.

Mkoa wote wa Kagera na majimbo yake yote kumi (10) ya uchaguzi tumekuwa tukipata wawakilishi kupitia chaguzi za serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu licha ya kwamba ufanisi wao kiutendaji umekuwa mdogo sana na usioridhisha kwa miaka yote kitendo kinachoumiza na kuisononesha jamii ya Wanakagera na hivyo kupelekea mdororo wa kiuchumi, kisiasa na kijamii mkoani humu.

Ndani ya Kagera na Halmashauri zake 8 tumekuwa na uongozi ndani ya vyama vya siasa kikiwemo chama Tawala (CCM) usiozingatia nguvu, ushiriki na thamani ya vijana wa mkoa huu kiasi cha kuendelea kukariri siasa na uongozi wa kiimla ndani ya mkoa wetu. Ni wakati sasa wa vijana wa KAGERA kuungana!

Tukirejea katika historia na asili ya Mkoa wetu wa Kagera, kipindi nchi yetu inapata uhuru mwaka 1961 Mkoa wa Kagera ulikuwa na Wilaya 4, ambazo ni Ngara, Biharamulo, Bukoba na Karagwe, Hizo wilaya Nyingine zimekuja kuongezeka baada ya uhuru kuaksi hali ya mabadiliko na ukuaji wa kijamii kwa kipindi hicho hadi hivi sasa.

Licha ya Mageuzi yote yaliyofanyika Mkoani Kagera toka enzi za kupata Uhuru hadi hivi sasa bado mkoa wetu huu umeendelea kudorora na kuendelea kupata maendeleo mgando (Stagnant Development Standards) yasiyolingana wala kuendana na hadhi ya mkoa wetu. Vijana tumekuwa tukiwekwa kando katika masuala ya maamuzi kama vile sisi siyo sehemu wala tunu ya mkoa wetu. Hii hali imekuwa ikitutafuna kama mkoa kiasi cha kuendelea kuruhusu akili ndogo kuongoza akili kubwa kisa tu ni wakongwe wa mkoa na wazoefu wa uongozi na utawala ndani ya mkoa huu. Ni wakati wetu sasa wa Vijana wa Kagera kuungana!

Mkoani Kagera, tumekuwa na waheshimiwa Madiwani, na Wabunge wengi ambao kwa nafasi walizonazo na walizowahi kupata hawakuwahi kuwaza kufanya mapinduzi ya maksudi katika kuondoa mkwamo wa kiuchumi katika jamii zetu. Ni wakati sasa wa vijana kuungana katika kuchochea mapinduzi ya maksudi ya kisiasa ambayo yatatupeleka kwenye kiu yetu ya maendeleo endelevu ya mkoa wetu. Katika hili hatupaswi kuendelea kuwa machawa na kuwasifia wanasiasa waliopo katika mambo ambayo hawajawahi kufanya vizuri. Hii itakuwa ni aibu na kujidharirisha sisi kama vijana wa Kagera.

Mkoani Kagera tumewahi kujaaliwa kupata Mawaziri, tumepata manaibu waziri, tumepata Makatibu wa Bunge, hadi Katibu wa Bunge aliyepo kwa sasa ni wa Kagera, tuna wabunge ambao hadi sasa wapo kwenye kamati mbalimbali katika wizara tofauti tofauti lakini mchango wao umekuwa na tija kiasi gani katika kuubadilisha mkoa wetu huu? Hili nalo linafikirisha.

Wabunge wa Mkoa wa Kagera wanaumoja wao ukiongozwa na Mheshimiwa Mwijage, lakini leo ukiwauliza ni kitu gani cha maana wamefanikiwa kukitekeleza kwenye mkoa wetu kwa kivuli cha umoja wao na kuipa jamii Matunda, watakupiga siasa. Kwanini tusipate sababu ya kuwakataa ? Vijana tuungane kuwakumbusha wale wanaothubutu na kuwakataa wale wasiowajibika, sasa ni wakati wetu!

Juzi kati hapa nimepata update ya kikao cha RCC hususani kwenye suala la Wahamiaji Haramu nikazidi kuuona ushindi wa vijana wa Kagera moyoni mwangu. Haiwezekani Mkoa wenye Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye pia kikanuni ni mjumbe wa RCC lakini bado masuala madogo kama hayo wanadodosa dodosa. Kama watawala wameshindwa kupata mwarobaini wa matatizo madogo kama hayo kwa mkoa wetu kwanini wasitulie sisi vijana tukawaelekeza njia ? Sisemi hivi kuwadharau watawala na viongozi waliopo, ila maana yangu ni kwamba mkoa wa Kagera unahitaji ICONS zenye uchungu na mkoa huu na wenye kujali maslahi ya jamii kuliko maslahi binafsi. Hili kwasasa wanaliweza vijana wa Kagera kwa Asilimia 100%. Kesho yetu ni Leo, Ni muhimu kuungana.

Vijana wa Kitanzania (na wa Kagera tukiwemo) kwasasa tunatambua kuwa tunalindwa na kuongozwa na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007 Toleo la 2024 ambayo ndiyo sera pekee iliyobeba maono na ukombozi wa kijamii na kitaifa kupitia vijana. Leo hii sera hii imetupwa kapuni kinachoongelewa ni UVCCM, BAVICHA n.k, kwanini tukubali kugawanyika na kuyaacha maono yetu kisa itikadi za kisiasa ? Vijana wenzangu wa Kagera tuwe wanasiasa wenye kulinda misingi ya vyama na umoja wetu huku msingi wa ujana na Mapinduzi ya kweli vikibaki kama nguzo kuu.

Vijana tunapaswa kutambua kuwa Mkoa wa Kagera una:-
Wilaya 8
Kata 192
Mitaa 66
Vijiji 662
Vitongoji 3,664

Orodha hii ni uthibitisho wa wazi kwamba Vijana tukiungana katika kusimamia Maeneo hayo hakika jamii tunaweza kuivusha pakubwa sana. Kesho yetu ni Leo Vijana, tuungane kuwakataa wanasiasa wababaishaji!

Vijana wa KAGERA, bila kujalisha itikadi zetu za kisiasa, kidini, kikabila, kikanda, kijamii n.k tuungane kwa pamoja KUSHIRIKI KATIKA UCHAGUZI MKUU UJAO ILI TUWEZE KUPATA TIKETI YA KUITUMIKIA JAMII YETU NA KUUJENGA MKOA WETU!

Vijana tunahitajika kwenye WDC,s
Vijana tunahitaji kwenye Baraza la Madiwani (H/W)
Vijana tunahitajika Bungeni
Vijana tunahitajika DCC’s
Vijana tunahitajika RCC’s
Vijana tunahitajika kwenye Kamati za Bunge
Vijana tunahitajika kwenye Wizara
Tuungane kwa pamoja kuujenga Mkoa wetu!

NB: Vijana wa Kagera hatushindani na Mtu, tunashindana na Ndoto zetu na kiu ya kuujenga mkoa wetu.

Kagera ipo toka 1947, hivyo ni kubwa kuliko sisi Vijana. Hivyo ni kubwa kuliko sisi.

Tuungane kuilinda na kuondoa Madarakani viongozi uchwara wasio na maono kwa ustawi wa Kata zetu, Majimbo yetu kwa mstakabali imara na thabiti wa mkoa wetu wa Kagera.

Amani na Maendeleo!
Umoja na Mshikamo!
Upendo na Uvumilivu!
Vijana na tuamke, kufanya mapinduzi ya kisiasa tuendeleze Mkoa wetu Kagera!

Abasole Twashiz’intahe, Ikigihe nichiwachu nyene!💪🏻🔰🇹🇿

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *