MBUNGE DOTTO BAHEMU AFIKISHA KERO YA UMEME KWA WAZIRI WA NISHATI.

By Na Mwandishi May 11, 2026

Na,Juventus Juvenary

Juzi Jumamosi Mei 09, 2026, Waziri wa Nishati Deogratius J. Ndejembi amefanya ziara Wilayani Ngara mkoani Kagera Region kwa lengo la kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika sekta ya nishati.
Katika ziara hiyo, Waziri Ndejembi ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Benaco hadi Kyaka pamoja na kituo cha kupoza umeme cha Benaco, mradi unaotarajiwa kuongeza upatikanaji na uhakika wa huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera.
Akizungumza mbele ya wananchi, Mbunge wa Jimbo la Ngara Dotto Jasson Bahemu amewasilisha kero na salamu za wananchi kwa Waziri wa Nishati, akieleza matumaini ya wananchi kuona changamoto za muda mrefu zikitatuliwa kupitia ujio wa miradi hiyo.
Miongoni mwa hoja zilizowasilishwa na Mbunge huyo ni pamoja na:
Changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ngara.
Madai ya wafanyabiashara waliotoa huduma na zabuni katika mradi wa umeme wa Rusumo.
Kipaumbele kwa wananchi wa Ngara kupata ajira na vibarua katika utekelezaji wa miradi ya umeme inayoendelea.
Akijibu hoja hizo, Waziri Ndejembi amewahakikishia wananchi kuwa serikali imezipokea changamoto hizo na itaendelea kuzifanyia kazi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya umeme pamoja na kunufaika na miradi inayotekelezwa katika eneo hilo.