Na, Juventus Juvenary – Ngara
Mbunge wa Jimbo la Ngara, Mheshimiwa Dotto Jasson Bahemu, ameshiriki ziara ya Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, pamoja na mkutano wa hadhara uliofanyika Benaco, Kata ya Kasulo, Wilaya ya Ngara, ambapo amewasilisha agenda mbalimbali za maendeleo zinazolenga kuboresha miundombinu na huduma kwa wananchi.
Miongoni mwa agenda alizowasilisha ni ombi la Serikali kuharakisha ujenzi wa barabara ya Nyakahura–Murusagamba–Rulenge–Murugarama kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo.
Mheshimiwa Bahemu amesema ujenzi wa barabara hiyo utakuwa na umuhimu mkubwa, hasa wakati Serikali ikitarajia kusaini mkataba wa uchimbaji wa madini ya Nickel, kwani utarahisisha mawasiliano, usafiri na shughuli za kiuchumi kuelekea eneo la mgodi.
Katika mkutano huo, Mheshimiwa Bahemu pia amesema Serikali imetenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa Kivuko cha Mayenzi–Kanyinya, fedha ambazo zitatatua changamoto ya usafiri kwa kuunganisha Kata za Kibimba na Mbuba.
Akijibu hoja zilizowasilishwa na Mbunge, Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, ameahidi kuzifanyia kazi na kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo ya Jimbo la Ngara.







