MBUNGE RUHORO NDAISABA ADAIWA KUWADHARAU WANANCHI WA NGARA
Na Mwandishi Wetu – Kasulo, Ngara
Baadhi ya wananchi wa Jimbo la Ngara wamemshutumu Mbunge wao, Ruhoro George Ndaisaba, kwa matamshi na mienendo ya dharau dhidi ya waliompa kura, wakisema kiongozi huyo amegeuka kuwa kero badala ya matumaini waliyokuwa nayo wakati wa uchaguzi uliopita.
Akizungumza kwa masikitiko, mmoja wa wananchi wa Kata ya Kasulo amenukuliwa akisema:
“Sisi tulimchagua bila hata kumfahamu. Hakuwa anajulikana kabisaaaaa!”
Kwa mujibu wa wananchi hao, Mbunge Ndaisaba amekuwa akijitapa hadharani kuhusu utajiri wake, akijinasibu kuwa ana magari ya kifahari, nyumba Ngara na Dar es Salaam, huku akiwaona wapiga kura kama watu wa daraja la chini.

Dharau kwa Wananchi na Viongozi
Inadaiwa kuwa mbali na kujigamba kwa mali, amekuwa pia akiwaudhi viongozi wa CCM ngazi ya wilaya kwa matamshi ya dharau na vitisho visivyo vya kisiasa. Vitendo hivi vinaelezwa kuleta mgawanyiko mkubwa ndani ya chama na jamii kwa ujumla.
“Hii si CCM tunayojua. Mbunge kijana anapaswa kuwa kiungo cha mshikamano, si chanzo cha kejeli kwa waliomtuma,” alisema mzee mmoja wa kata ya Rulenge.
Wito kwa Uongozi wa Chama na Serikali
Wananchi wameiomba CCM ngazi ya Mkoa na Taifa kuingilia kati kwa haraka, ili kudhibiti lugha na mienendo inayodhoofisha hadhi ya chama pamoja na kuumiza hisia za waliompa dhamana ya kuwatumikia.
“Madharau kwa wananchi ni kuvunja kiapo cha uwakilishi. Tunataka heshima irudi Ngara.”