MBUNGE WA NGARA NDAISABA RUHORO KUHUSISHWA NA UBAGUZI WA KISIASA NDANI YA CCM
‎Na Mwandishi Wetu – Ngara
‎
‎Mbunge wa Jimbo la Ngara, Mheshimiwa Ruhoro George Ndaisaba, anatuhumiwa kwa vitendo vya ubaguzi wa kisiasa vinavyodaiwa kuhatarisha mshikamano na demokrasia ya ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, huku wanachama wakimtaka uongozi wa juu wa chama kuingilia kati kabla ya mambo kuharibika zaidi.
‎
‎Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wanachama wa CCM wilayani Ngara, ambao hawataki majina yaandikwe hadharani mbunge huyo amekuwa akijihusisha na matendo ya kuwapendelea baadhi ya wagombea wa nafasi za udiwani kwa mwaka 2025, huku akiwadhalilisha kwa maneno viongozi na wanachama wengine wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
‎

‎Madhara ya Vitendo Vya Ubaguzi
‎Wanachama wamedai kuwa vitendo hivyo vina athari kubwa kwa chama, ikiwa ni pamoja na:
‎
‎Kugawanya wanachama wa CCM kwa misingi ya upendeleo, hali inayodhoofisha mshikamano na uaminifu miongoni mwa wanachama.
‎
‎Kuharibu demokrasia ya ndani ya chama, kwa kuvuruga mchakato wa ushindani wa haki.
‎
‎Kudhoofisha imani kwa uongozi wa CCM kitaifa, kwani viongozi wa juu wanatuhumiwa kufumbia macho mwenendo huo.
‎
‎Kuzorotesha utekelezaji wa Ilani ya Chama, kwa kuwa mikutano mingi imegeuzwa majukwaa ya kejeli na matusi.
‎
‎Kuvunjia heshima viongozi wastaafu, akiwemo Dkt. Philemon Sengati (Mkuu wa Mkoa mstaafu), Stephen Kagaigai (Katibu wa Bunge wa zamani) na Alex Gashaza (Mbunge mstaafu).
‎
‎Kukuza chuki na visasi vya kisiasa, hali inayosababisha hofu na migawanyiko ndani ya chama.
‎
‎Kuhatarisha ushindi wa CCM katika uchaguzi wa 2025, kwani wanachama wengi waliokata tamaa huenda wakajitoa au kutoshiriki kikamilifu kwenye shughuli za uchaguzi.
‎
‎Wanachama wameeleza kuwa baadhi ya viongozi wa chama wilayani humo wanadaiwa kushiriki katika vitendo hivyo vya upendeleo, akiwemo Suleiman Zubair, Mathias Mgatha, Staford Kenedy, Mukiza Byamungu na Bulindori Adonis.
‎

‎Wito kwa Uongozi wa CCM
‎”Chama hiki ni cha wanachama wote, si mali ya mtu mmoja au kikundi cha watu wachache. Tunalitaka Taifa na Mkoa kuchukua hatua haraka,” ilisomeka sehemu ya taarifa yao.
‎
‎Wanachama hao wanatoa wito kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera na Sekretarieti ya NEC Taifa kuchunguza kwa kina tuhuma hizi ili kurejesha maadili, haki na umoja ndani ya chama.
‎