Kiongozi asiye na Maono ni mzigo kwa anaowaongoza

By Titho Philemon Aug 4, 2024

Imekuwa ni dhana ya muda mrefu ambayo imejengeka miongoni mwa wanajamii wasiokuwa na uelewa wa mambo kwamba, kiongozi bora ni yule anayetoa hela, vijizawadi na kuwashughulisha wananchi katika burudani binafsi zenye lengo la kumpaisha na kumuinua kisiasa jambo ambalo siyo kweli.

Kiongozi bora anapaswa kuwa mtu mwenye uwezo wa kusimama imara katika kujali, kulinda, kutetea na kuhubiri upendo na mshikamano wa kijamii wa wale anaowaongoza.

Kiongozi anapaswa kuwa na maono chanya ambayo kwa namna moja ama nyingine yanamfikirisha na kumtafakarisha katika kuchambua kule alikotoka, mahali alipo na hatima kuhusu kule anakoelekea na kuwapelekea watu wake. Kiongozi wa aina hii anapaswa kwa dhati ayape kipaumbele maslahi ya jamii yake anayoiongoza na maslahi yake binafsi yawe ya ziada. Huo ndio uzalendo wa kweli.

Kiongozi asiye na Maono ni mzigo kwa wale anaowaongoza. Unakuta kiongozi anashinda anahamasisha vikundi vya kijamii ili viweze kumpatia uungwaji mkono kwenye mlengo wa kisiasa na kusahau jukumu lake la Msingi la kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Chonde Chonde wanajamii, tunakoelekea kwenye Chaguzi za 2024/2025 tujiweke tayari kuchagua viongozi wenye sifa sitahiki katika kutongoza bila kujalisha alikuwa katika mlengo upi wa kiitikadi kisiasa. Hii itatusaidia kupata jamii inayoheshimiana na viongozi wake na siyo kuwatenga wananchi kimafungu mafungu kama nyanya wakati wote ni wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mungu Ibariki Ngara!

Mungu Ibariki Tanzania!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *