Migogoro ya Ardhi Mamlaka ya Mji mdogo wa Rulenge – Ngara nani alaumiwe ?

By Titho Philemon Oct 5, 2024

Sheria ya Ardhi No. 4 ya Mwaka 1999 Sura ya 113 Toleo la 2019 ndiyo Sheria mama kwenye maswala ya Ardhi ikiwa na maana ya kwamba sheria nyingine hutungwa zikitokana na msingi wa Sheria hii.

Mamlaka ya Mji mdogo wa Rulenge ni Moja kati ya maeneo machache ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ambayo imezingatia mpango wa Matumizi bora ya Ardhi na kutenga maeneo ya Wakulima na Wafugaji.

Wafugaji wa Mtaa wa Munjebwe “A” na “B”, Mtaa wa Mubusoro, Mtaa wa Murubanga pamoja na maeneo ya jirani ambao walikuwa wanatumia Eneo la Machungio (Pasture) lililotengwa na Serikali kwenye Mamlaka hiyo kwasasa hawafurahii haki hiyo kwakuwa kuna vigogo wamenunua maeneo hayo na wengine TAYARI kuanza kuyalima!

Diwani wa Kata ya Rulenge Mjini Mr. Niyonzima, Township Executive Officer (TEO) wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Rulenge, Mwenyekiti wa Mtaa wa Munjebwe “A” na “B”, na Mwenyekiti wa Mtaa wa Murubanga ndani ya mamlaka hiyo na Bwana Mifugo wanapaswa kufuatiliwa kwa undani ili kujua ni sababu ipi imewafanya waendelee kukaa kimya na kulea uovu huo katika maeneo yao huku wafugaji wengi wakiendelea kuteseka kwa kukosa mahala salama na sahihi kwaajili ya kuchungia Mifugo yao.

Kitendo cha Wafugaji kuzibiwa njia (Free zones) ambazo zilikuwa zikitumiwa kwa wao kuvushia Mifugo yao kwenda kwenye malisho na manywesho kinaibua maswali kadhaa:-

  1. Nani aliyetoa kibali cha watu kulima katika maeneo ya Mapanda (Free zones) wakati yalishatengwa kwa ajili ya kupitishia Mifugo kwenda malishoni na manyweshoni ?
  2. WAJIBU wa Diwani kama Mwenyekiti wa Maendeleo ya Kata yake ya Rulenge ni yapi ? Je anatambua WAJIBU wake ? Na yeye NIYONZIMA kama kiongozi alichukua hatua gani baada ya kuona kwamba maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji yametumiwa kinyume na mpango kazi wake ?
  3. Mwenyekiti na Mtendaji wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Rulenge kama wahusika wa kuu kwenye kutathimini na kutolea maamuzi shughuli zote za Maendeleo ndani ya mamlaka hiyo ya Rulenge, wametoa kauli gani ili kuonesha msimamo wao katika kuwatetea wananchi hao wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Rulenge hususani wafugaji?
  4. Taarifa zilizopo ni kwamba, viongozi wa wilaya walishawahi kufika kwenye maeneo yenye migogoro ya Ardhi ndani ya mamlaka ya Mji mdogo wa Rulenge, Je walishafanya tathmini ya maeneo yenye shida na migogoro ya muda mrefu likiwemo eneo ambalo kwasasa liko chini ya Ndugu Erick Nkilamachumu (Diwani wa Bukiriro)?

Nikiwa ninatambua kuwa Sheria za Ardhi zote zimewekwa wazi kwaajili ya kuwasaidia wananchi, inapaswa sasa mamlaka za wilaya na za kikanda zenye uwezo wa kufanya maamuzi magumu katika hili ziingilie kati.

Binafsi kama kijana siwezi kuridhika nafsini kama wananchi hususani wafugaji kuendelea kuteseka na kuwa watumwa katika Ardhi yao wenyewe wakati matatizo mengine yanatatulika.

Katika hili ninapendekeza na kushauri yafuatayo:-

  1. Mamlaka za wilaya zipitie upya mipaka ya Free zones zilizotengwa kama njia kwa wafugaji kupitishia Mifugo yao ili yule atakayebainika amelima na kununua maeneo hayo aweze kunyang’anywa (Since “he’s illega Ab Initio”) na baadae yeye aweze kuchukuliana hatua na aliyemuuzia.
  2. Sheria ya Ardhi kwa mujibu wa kesi ya Farah Mohamed vs Fatuma Abdallah [1992] TZHC 21 (18 August 1992), pamoja na mambo mengine maamuzi ya Mahakama Kuu yalikuwa ni kwamba “Kama hauna hati halali /nzuri ya kiwanja hauwezi kumpatia mwezako hati nzuri/halali ya kiwanja (If you have a good and valid title you can not pass a good and valid title to the other). Tukija kwa upande wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Rulenge, wote walionunua Ardhi kwenye maeneo yote yaliyotengwa kwaajili ya kupitisha mifugo (free zones) watakuwa WAMEFANYA KAZI BURE maana mauziano yao na ununuzi wao ni Ubatili mtupu toka mwanzo (Void Ab initio) kwahiyo WANAPASWA KUNYANG’ANYWA MARA MOJA.
  3. Wafugaji wa Rulenge wote wanaoathiriwa na kadhia hizi za Ardhi ikiwemo kero hii ya kuzibiwa njia ya kuvusha Mifugo pamoja na kero nyingine zote wanapaswa KUTOKUPOA na kuhakikisha wanazisumbua mamlaka bila wasiwasi na kwa ustaarabu ili kile wanachoenda kudai kiweze kufikiriwa na kufanyiwa kazi ndio maana ofisi za umma zinakuwa wazi siku zote. Hofu yao ndo maumivu yao na jeuri kwa watawala.
  4. Halmashauri ya Wilaya ya Ngara imejitahidi sana kutenga maeneo na kuweka mabango kwamba eneo hili ni la Mifugo, hili la Makazi, hili la Zahanati, hili la Msitu na kadharika. Haipaswi kuishia hapo badala yake na maeneo yale mengine ambayo hayajatengewa njia za kupitishia Mifugo basi yatengwe ili kulinda barabara zetu zinazoharibiwa na Mifugo hususani msimu wa mvua unapoanza kama ilivyotengwa hiyo ya Rulenge. Hii itatusaidia sana.

Mwisho: Suala la Migogoro ya Ardhi kwa Ngara ni mtambuka kwahiyo kila mmoja wetu anapaswa kupewa elimu ya kutosha ili kutambua ni namna gani anaweza akailinda Ardhi yake na Ardhi ya wananchi wake (wenzake).

Tusimame imara katika kupigania kilichochetu ili jamii izidi kuwa salama na kuendelea kufurahia matunda ya ushirikiano na umoja wetu.

Rulenge Land Policies Must be subjected to Review!

Mungu ibariki Ngara!
Mungu ibariki Kagera!
Mungu ibariki Tanzania!

MUGIRE AMAHORO MEZA!🤲😑🧎‍♂️🙏

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *